Uwekezaji Tanzania

  • Mama Ameifungua Nchi: Miradi ya uwekezaji yaongezeka zaidi ya mara mbili

    Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai – Septemba) imeongezeka kufikia miradi 137 kutoka miradi 82 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 67. Aidha, ongezeko hilo limechochea pia kupata ongezeko maradufu la ajira zinazotokana na miradi ya uwekezaji kufikia ajira 86,986 ikilinganishwa na ajira 12,008 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2022/23, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 624. Matokeo ya kufurika kwa uwekezaji nchini Tanzania ni matunda ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuanzia kuwenye uboreshaji wa sheria, kanuni na taratibu, kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuimarisha amani na utulivu pamoja, matumizi ya TEHAMA na kurahisisha utoaji wa leseni na vibali. Pia, ziara za Mheshimiwa Rais Samia nje ya nchi zimechangia kuongezeka kwa uwekezaji nchini ambapo maeneo mengi anayokwenda amekuwa akiambatana na sekta binafsi ya Tanzania ambapo pia hukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa wa nchi anayokwenda, hivyo kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini, hatua inayowapelekea kuja kuwekeza nchini. Ongezeko hilo linafanya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa nchini kuanzia Januari hadi Septemba 2023 kufikia 366, sawa na asilimia 91.5 ya lengo la kusajili miradi 400 kwa mwaka huu. Miradi hiyo iliyosajiliwa hadi Septemba 2023 inatarajiwa kutoa ajira 116,986 pamoja na kuwekeza mtaji wenye thamani ya zaidi ya TZS trilioni 9.5 ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi. Lengo la Mheshimiwa Rais Samia na kuiwezesha Tanzania kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025. Read More

  • Mheshimiwa Rais aweka mikakati ya kuvutia uwekezaji wa trilioni 37 ifikapo 2025

    Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka wazi kuwa Tanzania inalenga kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025. Ameweka wazi mpango huo wakati akizungumza na wafanyabiashara wakubwa wa India katika jukwaa la uwekezaji la India na Tanzania jijini New Delhi ambapo amesema ili kufanikisha azma hiyo Serikali yake imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuboresha mfumo wa kisheria kwa kuufanya kuwa rafiki zaidi. Ameeleza kuwa Serikali yake inatambua umuhimu wa sekta binafsi na uwekezaji kama vichocheo vya ukuaji wa kiuchumi, hivyo mazingira ya biashara yameboreshwa ili kupanua biashara zilizopo na kuvutia uwekezaji mpya, jambo ambalo ni moja ya malengo ya ziara yake ya kimkakati nchini India. Kama sehemu ya mageuzi makubwa, Tanzania imeboresha matumizi ya teknolojia kuruhusu wawekezaji kusajili miradi popote pale duniani kupitia dirisha la kuhudumia wawekezaji kielektroniki, na hivyo kupata majibu kabla hata ya kutembelea Tanzania. “Tumepiga hatua kutoka kusajili uwekezaji wa dola bilioni 2 [TZS trilioni 5] mwaka 2020 hadi dola bilioni 5 [TZS trilioni 12.5] katika mwaka ulioishia Juni 2023. Lengo letu ni kufikia dola bilioni 15 kwa mwaka ifikapo mwisho wa 2025,” amesema. Tangu mwaka 1997 Tanzania imepokea jumla ya dola bilioni 3.87 za uwekezaji katika miradi 675 kutoka India ambayo imezalisha ajira zaidi ya 61,000, hivyo kufanya India kuwa miongoni mwa wawekezaji watano bora nchini Tanzania. Read More

  • Serikali ya matokeo: Thamani ya uwekezaji nchini yaongezeka zaidi ya mara mbili

    Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezeka kwa mwezi mmoja kufikia TZS trilioni 2.33 kwa Agosti mwaka huu kutoka TZS trilioni 1.06 kwa Julai mwaka huu, sawa na ukuaji wa asilimia 120. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji imeongezeka kufikia 58 kutoka 40 katika kipindi tajwa, ambapo kwa miradi iliyosajiliwa Agosti mwaka huu inatarajiwa kuzalisha ajira 25,700. Ongezeko la miradi limeendelea kusadifu mikakati na mkazo uliowekwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kilimo ili kuboresha maisha ya Watanzania ikizangatiwa sekta hii kwa takwimu za mwaka 2021 ilichangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, ilitoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Matokeo ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais imeendelea kuonekana ambapo thamani ya uwekezaji kwenye kilimo imeongezeka kwa zaidi ya TZS bilioni 275.53 kufikia TZS bilioni 849.13 kutoka TZS bilioni 571.1 kwa Julai mwaka huu. Wakati uwekezaji kwenye kilimo ukiendele kukua, Serikali imeendelea kuchua hatua kumwezesha mkulima mdogo ikiwemo kuimarisha huduma za ugani, kutoa ruzuku na pembejeo za kilimo, kufungua fursa za masoko, kujenga mifumo ya umwagiliaji, kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, hasa kwa vijana, pamoja na afua nyingine ili kuwezesha kilimo kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2030. Wanazuoni wamepongeza mageuzi yanayoendelea kufanyika kwenye kilimo ambapo Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kuwekeza zaidi kwenye kilimo, huku Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja amesema Tanzania inatambulika duniani kwa fursa nyingi kwenye kilimo. Read More

  • Mikakati ya Rais Samia unavyoweka rekodi ya uwekezaji Tanzania

    Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi ya uwekezaji 229 yenye thamani ya TZS trilioni 4.5 kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, ambapo lengo ni kufikia miradi 400 ifikapo Desemba 2023. Idadi hiyo inadhihirisha kasi kubwa ya usajili wa miradi nchini ikilinganishwa na miradi 293 iliyosajiliwa mwaka 2022, hivyo kusajili asilimia 78 ya miradi hiyo ndani ya nusu mwaka ni mafanikio makubwa kwa nchi. Kusajiliwa kwa miradi hiyo inayotoa ajira zaidi ya 30,000 kwa Watanzania katika sekta mbalimbali ni matokeo ya sera ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kuboresha sheria, kupunguza tozo/kodi mbalimbali na kuimarisha amani na utulivu. Aidha, takwimu zinaonesha mkakati huo wa Rais umefanikiwa zaidi kwani kwa miaka sita ya Serikali ya awamu ya tano, jumla ya miradi ya TZS trilioni 45 ilisajiliwa, huku miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita ikisajili miradi ya trilioni 22 ndani ya miaka miwili, takwimu zinazoonesha kuwa itafanya vizuri kuliko awamu iliyopita. Aidha, sababu nyingine ni taasisi 12 za usimamizi kuwa katika jengo moja hivyo kurahisisha utoaji huduma pamoja na matumizi ya TEHAMA yaliyorahisisha utoaji wa leseni na vibali mbalimbali vya biashara na uwekezaji hasa kupitia dirisha ya kielektroniki ambapo mwekezaji sasa anaweza kuwasilisha maombi akiwa popote dunia Read More

  • Mradi wa gesi asilia Lindi kutoa ajira za moja kwa moja 8,000

    Fursa za Watanzania kuendelea kunufaika na rasilimali zao zinaendelea kuongezeka ambapo awamu hii ni mradi kusindika gesi asilimia mkoani Lindi ambao unatajiwa kutoa ajira zaidi ya 8,000 kwa Watanzania pamoja na kuongeza matumizi ya nishati salama majumbani na maeneo mengine, kukuza uchumi na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine. Baada ya majadiliano yaliyodumu kwa takribani miaka miwili Tanzania na kampuni za uchimbaji wa mafuta na gesi za Equinor, Shell pamoja na Exxon Mobil zimefikia makubaliano kwa ajili ya uchimbaji wa gesi asilia, mradi ambao utagharimu zaidi ya TZS trilioni 70. Kupitia mradi huo ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza Juni 2025 mbali na ajira hizo za moja kwa moja, Watanzania zaidi watanufaika kwa ajira zisizo za moja kwa moja kwa kutoa huduma za kifedha, chakula na malazi, usafiri na usafirishaji, ulinzi, afya na mawasiliano. Aidha, kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwekezaji huo mikataba yote inayoingiwa itapitiwa na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri kama ambavyo Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ambapo mikataba mitano iliyoingiwa ikipitishwa na baraza itasainiwa Juni 2023. Mradi huo utaongeza mapato ya Serikali, Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC) litapata gawio kubwa, pia Watanzania watajengewa uwezo katika sekta ya gesi ikihusisha pia uhamilishaji teknolojia. Read More

  • Taarifa ya nafasi zaidi za ajira Januari – Machi 2023

    Tanzania imevutia uwekezaji wa TZS trilioni 2.8 katika kipindi cha miezi mitatu (Januari – Machi 2023) kutokana na mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa eneo bora la biashara na uwekezaji. Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) za Machi 2023 zinaonesha kuwa kutokana na miradi 93 iliyosajiliwa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/23, Watanzania watanufaika na fursa za ajira zaidi ya 16,400. Idadi hiyo ya uwekezaji ni ukuaji wa asilimia 48.9 ikilinganishwa na miradi ya uwekezaji wa TZS trilioni 1.8 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Aidha, ni ongezeko la asilimia 160 ikilinganishwa na uwekezaji wa TZS trilioni 1.1 uliosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021. Kwa miradi 37 iliyosajiliwa Machi 2023 pekee, nusu inamilikiwa na wazawa, huku wageni na ubia ikiwa ni asilimia 31 na asilimia 19 mtawala, hali inayoashiria kukua kwa uchumi na mazingira bora ya uwekezaji. Ziara ya Rais Samia nchini Afrika Kusini na ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris nchini Tanzania imetoa fursa ya kutangaza fursa za uwekezaji, ambapo kati ya kampuni 12 za Afrika Kusini zilizoonesha utayari wa kuwekezaji nchini, tayari moja imekuja kuangalia fursa za uwekezaji. Uamuzi wa Tanzania kurejea kwenye taasisi za kimataifa za usuluhishi pia umechangia kuongeza wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za usafirishaji, pamoja na ufanisi wa bandari. Read More

  • #MiakaMiwiliYaMama: Ajira za moja kwa moja Watanzania zaidi ya 85,000

    Mkakati wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuboresha mazingira ya biashara nchini na kuvutia uwakezaji umezaa matunda ambapo takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa thamani ya uwekezaji nchini umekua kwa asilimia 173. Ripoti ya TIC inaonesha kuwa thamani ya uwekezaji imepanda kufikia TZS trilioni 19.87 katika miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita, kutoka TZS trilioni 7.27 iliyorekodiwa katika miaka miwili kabla hajaingia madarakani. Ongezeko hilo ni matokeo ya kazi kubwa ya Rais ya kurejesha imani ya wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao amekuwa akikutana katika ziara zake nje ya nchi na ndani ya nchi ambapo pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji, pia alizipatia ufumbuzi changamoto zilizowakabili. Kati ya Machi 2021 na Februari 2023 idadi ya miradi iliyosajiliwa imeongezeka kutoka 455 hadi 575, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 26. Kati ya miradi hiyo, asilimia 32 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 42 ni ya wageni na asilimi 27 ni ubia kati ya wageni na wazawa. Kutokana na uwekezaji huo, idadi ya ajira zilizozalishwa kwa Watanzania zimeongezeka kutoka 61,900 hadi 87,187, uwekezaji mkubwa ukiwa kwenye sekta za viwanda, ujenzi wa majengo ya kibiashara na usafirishaji. Mafanikio haya yamehusishwa pia na Tanzania kushiriki katika mikutano ya kimataifa. Read More

  • Rais Samia: Uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 5 mwaka 2023

    Kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika nchini kwa kuboresha mazingira ya biashara kupitia mabadiliko ya kisheria na kanuni, ujenzi wa miundombinu na uainishaji maeneo muhimu kwa uwekezaji na biashara, uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2023 unatarajiwa kukua kwa asilimia 5 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022. Akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ambapo kwa kipindi kifupi cha Julai hadi Novemba kilishuhudia ongezeko la asilimia 22 la miradi iliyosajiliwa nchini kwa kipindi hicho kufikia miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 ambayo itatoa ajira 21,297. “Mabadiliko mbalimbali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Blueprint) yamechochea ukuaji wa sekta binafsi na kurejesha nguvu ya soko na kupunguza mwingilio wa serikali katika shughuli za kiuchumi, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa uwekezaji nchini,” amesema Rais Samia. Mkakati wa Rais Samia wa kuimarisha sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa kunawezesha kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa vijana wengi kujiajiri na kuajiri kupitia sekta hiyo, kwani takribani vijana milioni 1 huingia kwenye soko la ajira nchini kila mwaka, idadi ambayo Serikali pekee haiwezi kuwahudumia. Kupitia ujenzi wa miradi ya kimkakati unaoendelea nchini ikiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), reli ya kisasa, ujenzi na ukarabati wa meli mbalimbali, bomba la mafuta (EACOP) na mradi wa kuchakata gesi asilia mkoani Lindi, anaamini kuwa uchumi wa Tanzania utaendelea kuimarika na kuwanufaisha Watanzania zaidi. Wakati huo huo, amesema ana imani kuwa kila Mtanzania anayo nafasi katika maendeleo na mustakabali wa Tanzania na kuwa wananchi wanahaki na uhuru ambao wanastahili kuufurahia kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo nchini. Read More

  • Mkakati wa kibiashara wa Mheshimiwa Rais Samia wavutia uwekezaji wa TZS trilioni 7 nchini

    Mkakati wa kibiashara wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan unaendelea kuwa na matokeo chanya katika dira ya Serikali ya kukuza uchumi ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezaka karibu mara tatu ndani ya kipindi cha miezi mitano. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa taarifa inayoonesha kuwa kimesajili miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu ambapo sekta ya viwanda, usafirishaji na utalii ndizo zimeongoza kwa uwekezaji. Usajili huo ni ongezeko la miradi 24 kutoka miradi 108 yenye thamani ya TZS trilioni 2.06 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021. Miradi hiyo ambayo imeongezeka kwa idadi na thamani, itatoa ajira 21,297 ambazo ni ongezeko la asilimia 57 kutoka ajira 13,578 za mwaka jana ni matokeo ya Diplomasia ya Uchumi ambayo Rais amekuwa akiitekeleza kwa vitendo. Rais Samia ameendelea kuimarisha mahusiano ya kibiashara ndani ya nchi, kikanda na kimataifa katika ziara mbalimbali anazofanya ambazo huambatana na wafanyabiashara wa ndani ambao hupata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara wa nje, lakini pia huwezesha Tanzania na nchi nyingine kuingia makubaliano ya kibiashara na uwekezaji. Tangu aingie madarakani Rais amefanikiwa kurejesha imani ya wawekezaji ambao sasa wanaamani ya kuja na kuwekeza nchini. Katika muda huo ametatua changamoto mbalimbali za kibiashara kama vile kupunguza muda wa kupata vibali vya uwekezaji, kurekebisha mifumo ya kikodi, kuondoa ukiritimba wa vibali vya kazi na kuwepo kwa maeneo maalum ya uwekezaji. Read More