December 2023
-
Mtaji wa uwekezaji ya wazawa umefikia wastani wa asilimia 50 ya miradi yote iliyosajiliwa kila mwezi, ikiwa ni matokeo ya mwaka mmoja tu baada ya serikali kupunguza kiwango cha mtaji wa uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani, kutoka dola za Kimarekani 100,000 (shilingi milioni 250) hadi dola za Kimarekani 50,000 (Shilingi milioni 125). Mafanikio hayo chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ni matokeo ya maboresho ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022 ambayo imeweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji, mifumo ya kitaasisi, ulinzi, vivutio, kutoa motisha na kurahisisha uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) miradi ya uwekezaji wa ndani ilichangia wastani wa asilimia 20 ya miradi yote kabla ya kutekelezwa kwa sheria mpya ambapo mwaka 2021 Tanzania ilikuwa na miradi yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2 bilioni iliyosajiliwa, lakini kwa mwezi Agosti pekee mwaka huu, Tanzania imesajili miradi yenye thamani ya takribani dola za Kimarekani bilioni 1. Ongezeko la uwekezaji wa ndani linatoa matumaini mapya nchini kwa kuimarisha sekta binafsi, kupunguza changamoto za ajira na kuongeza ushawishi kwa wa ushirikiano na kampuni za nje zinazohitaji ubia na kampuni za ndani zenye uhakika wa mtaji. Aidha, sheria hiyo inatoa ahueni kubwa zaidi kwa wawekezaji wazawa kwani endapo hana fedha inayofikia kiwango husika, lakini thamani ya mali aliyonayo, mfano shamba, mashine au malighafi nyingine ambazo zinafikia thamani hiyo anaweza kusajiliwa na TIC na kunufaika na vivutio vya uwekezaji. Read More
-
Katika kuendelea kufungua fursa za ajira ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetangaza neema ya uwepo wa ajira 500 za wauguzi wa kike kuajiriwa na Serikali ya Saudi Arabia mapema Januari 2024. Ajira hizo ni matokeo ya Mheshimiwa Rais Samia kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani, ambapo mwishoni mwa Novemba na mwanzoni wa Desemba 2023 Tanzania imesaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya kazi na ajira na Saudi Arabia pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu. Hati hizo zinatoa fursa za ajira kwenye mataifa husika kwa kada na sekta zenye kutumia ujuzi wa chini, ujuzi wa kati na ujuzi wa juu na pia zinaweka utaratibu rasmi wa kuratibu ajira za Watanzania wanaoenda kufanya kazi nje, ili kuhakikisha wajibu na haki za zao zinalindwa na kuzingatiwa ipasavyo. Alisema watanzania wote wenye sifa na ujuzi uliobainishwa wanataarifiwa kuomba kazi husika kwa kujisajili https://jobs.kazi.go.tz na kutuma wasifu binafsi (CV) kwa njia ya barua pepe esu@taesa.go.tz, ambapo mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 27, 2024. Wakati huo huo, Serikali inaendelea kufanya mashauriano katika hatua mbalimbali na nchi nyingine zaidi ya 10 kwa lengo la kuwa na makubaliano ya ushirikiano utakaowezesha Watanzania kunufaika na fursa za ajira kwenye nchi husika. Read More
-
Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imetenga eneo lenye rutuba la ukubwa wa hekta 60,103 kwaajili ya mji wa kilimo (kilimo kikubwa cha kibiashara pamoja na ufugaji wa kisasa) litakalotolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Eneo hilo lipo Mkulazi mkoani Morogoro, pembezoni mwa reli ya TAZARA na linafaa kwaajili ya kilimo cha miwa, mpunga, mahindi, mtama na mengineyo. Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inakusudia kupunguza uagizaji wa mazao kutoka nje, pamoja na kuwa kapu la chakula la kulisha nchi nyingine. Kilimo cha miwa kitaongeza malighafi kwenye viwanda vya uzalishaji wa sukari na hivyo kuiwezesha nchi kuachana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Tanzania iliagiza tani 30,000 za sukari ili kufidia nakisi ya uzalishaji wa ndani. Mashamba manne (kila moja likiwa na ukubwa wa hekta 10,000) zitatumiwa kwa ajili kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na aina ya udongo, shamba jingine lenye ukubwa wa hekta 10,000 litatengwa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na usindikaji wa mazao ya mifugo, huku hekta 10,103 zilizobaki zikihifadhiwa kwa matumizi ya baadaye kwa ajili ya kuanzisha maeneo ya usindikaji wa bidhaa za kilimo na viwanda vya kuongezea thamani bidhaa za kilimo. Katika hatua nyingine ya kuvutia uwekezaji, TIC imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 3,200 mkoani Kigoma kwa ajili kilimo cha michikichi, usindikaji wa mawese na kilimo cha mazao mengine. Hatua hii pia itaiwezesha nchi kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula ambapo kwa takwimu za sasa 60% ya bidhaa hiyo muhimu inatoka nje ya nchi ikiigharimu nchi zaidi ya TZS bilioni 627 kwa mwaka. Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa Tanzania imetumia 33% tu ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo, hivyo kuwa na fursa kubwa ya kujikuza kupitia kilimo cha kibiashara, ambapo sasa serikali imeweka mkakati wa kuifungua. Read More
-
Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa dira mpya ya Taifa ya maendeleo ya miaka 25 (mwaka 2025 hadi mwaka 2050) ambayo itakuwa ni dira ya pili kuandaliwa nchini baada ya ile iliyoanza mwaka 2000 na inatarajiwa kumalizika mwaka 2025. Akizindua mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandaa dira mpya, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameainisha maeneo nane ya kipaumbele katika dira mpya ambayo yanatokana na mahitaji ya sasa ya dunia, makosa na mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa dira inatoelekea ukomo pamoja na mahitaji mengine ya kitaifa. Kwanza, ukuaji wa uchumi kufungamanishwa na sekta za uzalishaji zinazowagusa wananchi wengi zaidi na kutengeneza ajira kwaajili yao kama vile sekta ya kilimo. Pili, kukusanywa kwa takwimu kutoka sekta isiyo rasmi ili kupata hali halisi ya uchumi badala ya kutumia takwimu za sekta rasmi pekee, hali inayosababisha kukosa uhalisia wa hali ya uchumi. Eneo la tatu ni tathmini na ufuatiliaji ambao utawezesha kubaini viashiria vya kasoro kwenye utekelezaji wa dira mapema na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha malengo yanafikiwa. Nne, uratibu wa kufungamanisha miradi ya kipaumbele kwa sekta zinazohusika katika uzalishaji. Katika hili Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa mipango ya sekta moja inapotekelezwa iwe na mwingiliano na mchango katika sekta nyingine ili kutumia rasilimali chache kwa matokeo makubwa. Tano, amesisitiza dira iweke mwelekeo wa uwekezaji na usimamizi wa maboresho ya kiutendaji wa mashirika ya serikali ili yaongeze ufanisi katika uendeshaji na yaweze kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa. Ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi ni eneo la sita alilolitaja ambapo amesema lazima sekta binafsi iimarishwe na iwe tayari kuimarika ili ziwe na uwezo na utayari wa kufanya biashara, kutengeneza ajira pamoja na kushirikiana na sekta binafsi nje ya nchi. Uimarishaji huo unajumuisha uwepo wa mifumo rafiki ya kisheria, upatikanaji wa mitaji na rasilimali watu yenye ujuzi. Kuzingatiwa kwa maadili ya Taifa ni sehemu… Read More
-
Kutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara na kupelekea vifo vya zaidi ya watu 50, kujeruhi wengine zaidi ya 80 pamoja na kuharibu makazi ya watu na mali mbalimbali, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amekatisha ziara yake iliyokuwa inaendelea Dubai. Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Dubai kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) amekatisha safari hiyo na anarejea nchini ili kushughulikia kwa karibu janga hilo. Aidha, ametoa maelekezo kuwa serikali igharamie mazishi ya wote waliofariki na majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama viendelea kutoa msaada wa dharura na uokoaji. Pia, ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao. Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza tathmini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida. Ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba mkubwa uliowakumba na pia amewahakikishia wananchi walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao na itahakikisha inashughulikia masuala yote yaliotokana na janga hili. Read More