Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai – Septemba) imeongezeka kufikia miradi 137 kutoka miradi 82 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 67.
Aidha, ongezeko hilo limechochea pia kupata ongezeko maradufu la ajira zinazotokana na miradi ya uwekezaji kufikia ajira 86,986 ikilinganishwa na ajira 12,008 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2022/23, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 624.
Matokeo ya kufurika kwa uwekezaji nchini Tanzania ni matunda ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuanzia kuwenye uboreshaji wa sheria, kanuni na taratibu, kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuimarisha amani na utulivu pamoja, matumizi ya TEHAMA na kurahisisha utoaji wa leseni na vibali.
Pia, ziara za Mheshimiwa Rais Samia nje ya nchi zimechangia kuongezeka kwa uwekezaji nchini ambapo maeneo mengi anayokwenda amekuwa akiambatana na sekta binafsi ya Tanzania ambapo pia hukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa wa nchi anayokwenda, hivyo kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini, hatua inayowapelekea kuja kuwekeza nchini.
Ongezeko hilo linafanya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa nchini kuanzia Januari hadi Septemba 2023 kufikia 366, sawa na asilimia 91.5 ya lengo la kusajili miradi 400 kwa mwaka huu. Miradi hiyo iliyosajiliwa hadi Septemba 2023 inatarajiwa kutoa ajira 116,986 pamoja na kuwekeza mtaji wenye thamani ya zaidi ya TZS trilioni 9.5 ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi.
Lengo la Mheshimiwa Rais Samia na kuiwezesha Tanzania kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025.