Taarifa ya nafasi zaidi za ajira Januari – Machi 2023

Tanzania imevutia uwekezaji wa TZS trilioni 2.8 katika kipindi cha miezi mitatu (Januari – Machi 2023) kutokana na mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa eneo bora la biashara na uwekezaji.

Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) za Machi 2023 zinaonesha kuwa kutokana na miradi 93 iliyosajiliwa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/23, Watanzania watanufaika na fursa za ajira zaidi ya 16,400.

Idadi hiyo ya uwekezaji ni ukuaji wa asilimia 48.9 ikilinganishwa na miradi ya uwekezaji wa TZS trilioni 1.8 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Aidha, ni ongezeko la asilimia 160 ikilinganishwa na uwekezaji wa TZS trilioni 1.1 uliosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021.

Kwa miradi 37 iliyosajiliwa Machi 2023 pekee, nusu inamilikiwa na wazawa, huku wageni na ubia ikiwa ni asilimia 31 na asilimia 19 mtawala, hali inayoashiria kukua kwa uchumi na mazingira bora ya uwekezaji.

Ziara ya Rais Samia nchini Afrika Kusini na ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris nchini Tanzania imetoa fursa ya kutangaza fursa za uwekezaji, ambapo kati ya kampuni 12 za Afrika Kusini zilizoonesha utayari wa kuwekezaji nchini, tayari moja imekuja kuangalia fursa za uwekezaji.

Uamuzi wa Tanzania kurejea kwenye taasisi za kimataifa za usuluhishi pia umechangia kuongeza wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za usafirishaji, pamoja na ufanisi wa bandari.