MAMA ni mwanamageuzi: Maboresho ya sheria yaongeza uwezo wa wazawa kuwekeza nchin

Mtaji wa uwekezaji ya wazawa umefikia wastani wa asilimia 50 ya miradi yote iliyosajiliwa kila mwezi, ikiwa ni matokeo ya mwaka mmoja tu baada ya serikali kupunguza kiwango cha mtaji wa uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani, kutoka dola za Kimarekani 100,000 (shilingi milioni 250) hadi dola za Kimarekani 50,000 (Shilingi milioni 125).

Mafanikio hayo chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ni matokeo ya maboresho ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022 ambayo imeweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji, mifumo ya kitaasisi, ulinzi, vivutio, kutoa motisha na kurahisisha uwekezaji nchini.

Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) miradi ya uwekezaji wa ndani ilichangia wastani wa asilimia 20 ya miradi yote kabla ya kutekelezwa kwa sheria mpya ambapo mwaka 2021 Tanzania ilikuwa na miradi yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2 bilioni iliyosajiliwa, lakini kwa mwezi Agosti pekee mwaka huu, Tanzania imesajili miradi yenye thamani ya takribani dola za Kimarekani bilioni 1.

Ongezeko la uwekezaji wa ndani linatoa matumaini mapya nchini kwa kuimarisha sekta binafsi, kupunguza changamoto za ajira na kuongeza ushawishi kwa wa ushirikiano na kampuni za nje zinazohitaji ubia na kampuni za ndani zenye uhakika wa mtaji.

Aidha, sheria hiyo inatoa ahueni kubwa zaidi kwa wawekezaji wazawa kwani endapo hana fedha inayofikia kiwango husika, lakini thamani ya mali aliyonayo, mfano shamba, mashine au malighafi nyingine ambazo zinafikia thamani hiyo anaweza kusajiliwa na TIC na kunufaika na vivutio vya uwekezaji.