Rais wa Tanzania
-
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameianzisha safari itakayoshuhudia mageuzi makubwa ya mashirika ya umma, taasisi na wakala za Serikali ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na kuziwezesha taasisi hizo kujiendesha kwa tija na ufanisi ili kupunguza utegemezo kutoka Serikalini. Mageuzi hayo yametokana na uhalisia kuwa licha ya wingi wa mashirika na wakala hizo (248) ambazo Serikali imewekeza mtaji wa TZS trilioni 73, bado mchango wake kwenye uchumi ni mdogo sana, kwani kwa sasa taasisi hizo zinachangia asilimia 3 tu kwenye bajeti ya Serikali, huku nyingi zikitegemea ruzuku ili kujiendesha. Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa maono ya Mwalimu Nyerere kuanzisha mashirika ya umma alitaka yamilikiwe na wananchi wenyewe kupitia hisa na kwamba wananchi washirikishwe kwenye masuala ya mashirika hayo, na hivyo ameagiza hatua zichukuliwe ili kurudi kwenye msingi huo. “Kwa kuwa kwa sasa wapo wananchi wenye uwezo wa kununua hisa, hata kama ni kidogo kidogo, nadhani turejee kwenye mwelekeo huo,” ameagiza. Ili kufikia malengo hayo, Mheshimiwa Rais ameridhia mabadiliko mbalimbali ambayo ni pamoja na kutoa uhuru kwa taasisi kujiendesha katika mambo ya msingi, kufanya maboresho katika taratibu za ajira kwa watumishi wao na katika sheria ya ununuzi wa umma, na kuongeza kusiwepo kwa kuingiliwa kisiasa kwenye utendaji wa taasisi hizi. Pia, Serikali ipo kwenye mchakato wa kutunga sheria itakayobadili hadhi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, na kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ili kuondoa utegemezi kutoka mfuko mkuu wa Serikali. Kutokana na uchunguzi uliobaini uwepo wa taasisi ambazo majukumu yake yanashabihiana au hayana umuhimu kwa sasa na zile ambazo zinalega lega Serikali itaziunganisha au kutatua changamoto zao ziwezeshe kujiendesha kwani mashirika hayo ni muhimu kwa uchumi zikiwa zinatoa asilimia 17 ya ajira zote nchini. Amewatoa hofu watumishi kuwa mabadiliko yatakayofanyika hayataathiri ajira zao… Read More
-
Katika kutelekeza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa mashirika na taasisi nyingine za Serikali au zile ambazo Serikali ina hisa nyingi zinajiendesha kwa faida, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechua ameainisha hatua tano za kimkakati ambazo zitachochea mabadiliko katika ufanisi wa taasisi hizo. Kwanza amesema ni kujenga utamaduni wa kukutana katika kikao kazi kila mwaka na watendaji na wenyeviti wa taasisi hizo. Pili, ni mabadiliko ya sheria ambayo yatahusisha kuondoa sheria zilizopitwa na wakati au zinazokwamisha mashirika kujiendesha kwa ufanisi. Hatua ya tatu ni kuangalia namna ya kuwapata viongozi wa kuendesha taasisi hizo ili kuhakikisha kuwa wanaopewa dhamana ni wenye ujuzi stahiki ambapo Mheshimiwa Rais amewahi kupendekeza kuwa nafasi hizo ziwe zinatangazwa, ili watu wenye sifa watume maombi. Nne ni uboresha wa bodi za taasisi hizo kwa kuangalia namna zinavyoteuliwa ambapo amesema lengo ni kuchagua watu wenye uwezo wa kiutendaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. Hatua ya tano ni kutoa uhuru kwa taasisi hizo kuajiri ambapo mchakato huo tayari umeanza na kwa hatua ya kwanza wanaanza na taasisi za kibiashara na vyuo vikuu. Mchechu amesema baada ya hatua hizi, hatua zaidi za kimabadiliko zitachukuliwa ndani ya taasisi moja moja na viongozi husika na kuwa lengo ni kuziwezesha kuwa na ufanisi, kuongeza faida na kutoa gawio serikalini ili kupunguza utegemezi wa ruzuku. Read More
-
Wakuu wa nchi za Afrika, viongozi wa ngazi mbalimbali na wadau wengine wamekusanyika Tanzania kujadili mustakabali wa rasilimali watu barani Afrika ambapo Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu ametumia jukwaa hilo kueleza hatua mbalimbali ambazo Tanzania imezichukua kuimarisha sekta hiyo ambayo ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za lishe na huduma za afya ya uzazi wa mama na mtoto. Hatua nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu ili kuondoa udumavu ambao, mara nyingi, hupunguza kiwango cha uelewa na uwezo wa kusoma kwa waoto na kuhakikisha watoto wanaandaliwa kimwili, kiakili, kiisimu/kijinsia kiubunifu na kiakili-hisia. Aidha, Serikali imetoa afua kwa kaya masikini, inatoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita, inapanua elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, imefuta ada kwa baadhi ya vyuo vya ufundi, imeanza kutoa mikopo kwa vyuo vya kati, inatoa mikopo kwa vijana, inaruhusu waliokatisha masomo kurejea shule pamoja na kuweka mkakati wa kuvutia vijana kwenye kilimo, yote haya yakilenga kuongeza mchango wao kwenye uchumi. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, vijana ndio kundi lenye watu wengi zaidi nchini Tanzania, hivyo hatua ambazo Rais ameeleza kuwa Tanzania imezichukua kwa asilimia kubwa zimewalenga vijana kwani anaamini kwamba maisha bora ambayo vijana wengi hukimbilia Ulaya kuyafuata yanaweza kupatikana barani Afrika endapo Serikali zao zitawawezesha. “Viongozi wenye maono hujenga sera zao kwenye maendeleo ya watu na kufuatiwa na maendeleo ya vitu,” amesema Rais Samia akitoa wito kwa viongozi wenzake wa Afrika na kusisitiza kwamba Afrika haitoweza kuendelea endapo rasilimali watu isipoendelezwa. Read More
-
Dhamira za dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta binafsi na kuhakikisha inashiriki katika kuchochea maendeleo ya wananchi inazidi kudhihirika kufuatia marekebisho yaliyofanyika kwenye Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023 ili kuondoa changamoto zilizosababisha ushiriki hafifu wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa ubia. Maboresho yaliyofanyika yataongeza kasi ya ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kupunguza muda wa maandalizi ya miradi na hivyo kuharakisha utekelezaji wa miradi ya PPP, hatua ambazo zitaipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti sambamba na kukuza sekta binafsi. Changamoto zilizotatuliwa ni pamoja na sheria kutotoa haki kwa wabia kutoka sekta binafsi kuwasilisha migogoro kwenye mahakama za kimataifa kwa utatuzi, kutoainisha aina ya misaada ya kifedha (public funding) itakayoidhinishwa kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada. Nyingine ni sheria kutoruhusu mamlaka za Serikali kufanya ununuzi wa moja kwa moja wa mbia kutoka sekta binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi inayoibuliwa na mamlaka hizo na kutoweka masharti kwa mwekezaji kutoka sekta binafsi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa PPP kuunda Kampuni. Tayari Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo barabara (Expressway) kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro, mradi ambao utaweka historia ya kuwa mradi mkubwa zaidi wa barabara kujengwa kwa kushirikiana na sekta binafsi. Read More
-
Hatua ya Bunge la Tanzania kupitisha azimio la kuridhia ushirikiano kati ya Tanzania na Dubai kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika uendelezaji na uboreshaji utendaji kazi wa bandari Tanzania ni hatua nyingine kubwa katika mkakati wa Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji Afrika Mashariki na Kati ndani ya muongo mmoja ujao. Kupitishwa kwa azimio hilo kunaipa nafasi Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Dubai kupitia Kampuni ya DP World kuanza majadiliano yanayolenga kuangazia namna ya kushirikiana ili kuongeza ufanisi wa bandari nchini, hasa Bandari ya Dar es Salaam ambayo imekuwa lango la kibiashara kwa nchi za Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini wa Afrika. Kufanikiwa kwa ushirikiano baina ya Serikali hizi mbili kutatimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ya kuongeza mapato ya bandari kutoka TZS trilioni 7.7 za sasa hadi TZS trilioni 26 ndani ya muongo mmoja, ambayo yataweza kufadhili shughuli za kijamii na kimaendeleo nchini, hivyo kupunguza utegemezi kwa washirika wa maendeleo, jambo ambalo ni msingi katika kudhihirisha Uhuru wa nchi kwenye kupanga na kuamua mambo yake. Mafanikio mengine ambayo Tanzania itayapata ni kuongezeka kwa ajira kutoka nafasi 28,990 za sasa hadi ajira 71,907, kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 hadi saa 24, kupunguza muda wa ushushaji makontena kutoka siku 4.5 hadi siku 2, kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 hadi saa 1, kupunguza gharama ya usafirishaji mizigo kutoka nje ya nchi kwenda nchi jirani kwa asilimia 50, pamoja na kuongeza shehena ya mizigo kutoka tani milioni 18 hadi tani milioni 47. Mbali na manufaa hayo, uendelezaji wa bandari pia utachochea ukuaji wa sekta nyingine kama uvuvi, kilimo, ufugaji, viwanda na biashara, usafirishaji (anga, reli, barabara), kiimarisha diplomasia pamoja na Watanzania kunufaika na teknolojia na ujuzi wa uendeshaji wa bandari kisasa. Ili kuendeleza uwazi na uwajibika, Serikali chini… Read More
-
Fursa za Watanzania kuendelea kunufaika na rasilimali zao zinaendelea kuongezeka ambapo awamu hii ni mradi kusindika gesi asilimia mkoani Lindi ambao unatajiwa kutoa ajira zaidi ya 8,000 kwa Watanzania pamoja na kuongeza matumizi ya nishati salama majumbani na maeneo mengine, kukuza uchumi na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine. Baada ya majadiliano yaliyodumu kwa takribani miaka miwili Tanzania na kampuni za uchimbaji wa mafuta na gesi za Equinor, Shell pamoja na Exxon Mobil zimefikia makubaliano kwa ajili ya uchimbaji wa gesi asilia, mradi ambao utagharimu zaidi ya TZS trilioni 70. Kupitia mradi huo ambao ujenzi wake unatarajiwa kuanza Juni 2025 mbali na ajira hizo za moja kwa moja, Watanzania zaidi watanufaika kwa ajira zisizo za moja kwa moja kwa kutoa huduma za kifedha, chakula na malazi, usafiri na usafirishaji, ulinzi, afya na mawasiliano. Aidha, kuhakikisha Watanzania wananufaika na uwekezaji huo mikataba yote inayoingiwa itapitiwa na kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri kama ambavyo Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ambapo mikataba mitano iliyoingiwa ikipitishwa na baraza itasainiwa Juni 2023. Mradi huo utaongeza mapato ya Serikali, Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC) litapata gawio kubwa, pia Watanzania watajengewa uwezo katika sekta ya gesi ikihusisha pia uhamilishaji teknolojia. Read More
-
Serikali imetangaza kuwa huduma za vipimo vya awali kwa wajawazito ambazo zinahusisha kupima wingi wa damu, mkojo ili kuangalia wingi wa protini, shinikizo la damu pamoja na kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto, zitatolewa bure. Kutolewa bure kwa vipimo hivyo muhimu kutawawezesha wajawazito kujua mwenendo wa ujauzito, kuepuka kifafa cha mimba na vifo vya mama na mtoto ambapo lengo la Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) ni kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 321 kwa vizazi 100,000, hadi vifo 220 na vifo vya watoto kutoka vifo 51 kwa vizazi hai 1,000 hadi vifo 40. Aidha, hatua hii itaongeza zaidi idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki pamoja na kujifungulia kwenye vituo vya afya ambapo Serikali imeahidi itahakikisha upatikanaji wa 100% wa dawa za kuzuia kutoka damu wakati wa kujifungua, dawa za kuongeza damu na dawa za kuzuia kifafa cha mimba katika vituo vyote afya vya umma. Hatua hizi ni mwendelezo wa kazi kubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu wa kujenga vituo vya afya, kuboresha miundombinu ya afya nchi nzima, kuajiri maelfu ya watumishi wa afya pamoja na kununua vifaa tiba, hivyo kuiarisha huduma za afya vijijini ambapo awali hali ilikuwa ngumu zaidi. Imani juu ya huduma za afya zinazoendelea kutolewa kwenye vituo vya afya imeendelea kuongezeka kwani kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya mwaka 2022, idadi ya wajawazito waliotembelea kliniki walau mara nne kati ya wajawazito 100 imeongezeka kutoka 53 mwaka 2015/16 hadi 65 mwaka 201/22 kati huku wanaojifungua chini ya uangalizi wa mtoa huduma mwenye ujuzi ikiongezeka kutoka 66 hadi 85 katika kipindi hicho. Read More
-
“Wafanyakazi mambo ni moto, mambo ni fire,” ni maneno aliyoyatumia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhitimisha hotuba yake ya Mei Mosi 2023 ambayo ilijaa matumaini kwa maelfu ya watumishi wa umma waliokuwa wameujaza uwanja wa Jamhuri Morogoro wakimsikiliza. Miongoni mwa mengi yaliyowafurahisha watumishi hao ambao wameendelea kushuhudia mabadiliko makubwa kwenye mazingira ya kazi na maslahi yao chini ya Rais Samia ni uamuzi wa Rais kurejesha nyongeza ya mishahara ya kila mwaka, ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa kwa mfumo huo. Itakumbukwa kuwa Mei 2022 Rais Samia aliridhia nyongeza ya mishahara ambapo alipandisha kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambapo TZS trilioni 1.59 zilitumika kwa ongezeko hilo kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Aidha, mbali na kurejesha utaratibu huo, Rais amesema kuwa nyongeza ya posho ambayo ilipandishwa mwaka jana lakini baadhi ya watumishi hawakuanza kuipata kwa sababu bajeti za taasisi zao tayari zilishapitishwa, wataanza kupata fedha hizo mwaka wa fedha ujao. “Tumejiandaa pia kupandisha madaraja, vyeo vitaendelea kupandishwa, kutenganisha makundi na madaraja mserereko wale ambao hawakupata mwaka jana watapata mwaka huu” ameahidi. Pia, alisema Serikali anayoiongoza itaendelea kuwekeza na kuvutia uwekezaji nchini, ili kujenga uchumi na kuzalisha ajira kwa Watanzania na zipatikane fedha za kuboresha maslahi ya watumishi. Read More
-
Licha ya kuwa ukuaji wa bara la Afrika unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2022 hadi asilimia 3.8 mwaka 2023, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua zaidi huku Umoja wa Mataifa (UN) ukiitaja kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi mwaka 2023. Tanzania ambayo inaendelea kuwa mfano Afrika kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, inatarajiwa kushuhudia ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.6, ikitanguliwa na Ivory Coast ambayo uchumi wake utakua kwa asilimia 6.5 pamoja na Rwanda itakayoshuhudia ukuaji wa asilimia 7.8. Mafanikio hayo ni matokeo ya mikakati ya Rais Samia ambapo katika miaka miwili ya uongozi wake amesajili miradi ya uwekezaji ya TZS trilioni 17, ambayo imechochea ukuaji wa sekta nyingine pamoja na kutoa fursa za ajira kwa maelfu ya Watanzania. Mikakati hiyo pia imewezesha uchumi kukabiliana na changamoto za dunia kama mfumuko wa bei, gharama kubwa za ukopaji na mabadiliko ya tabianchi. Wakati ripoti ya UN ikionesha hivyo, Benki ya Dunia (WB) imeitaja Tanzania kuwa nchi ya 10 kwa utajiri barani Afrika kwa kwa kuzingatia Pato Ghafi la Taifa (FDP) kwa kuangalia viwango vya sasa vya kubadili fedha. Ukuaji huo mbali na kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania lakini pia unawapa imani wawekezaji waliopo na wanaokusudia kuwekeza nchini, kwa kuwafanya waamini Tanzania ni sehemu salama kuwekeza mitaji yao ya mabilioni, hivyo kufanya uchumi kukua zaidi na zaidi. Read More
-
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetoa takwimu zinazoonesha kuongezeka kwa pato la Taifa la Tanzania kutoka Dola za Marekani Bilioni 69.9 (TZS trilioni 163.5 trilioni) kwa mwaka 2021, wakati ambapo Rais Samia alipoingia madarakani hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 85.42 (TZS trilioni 200) kwa mwaka huu wa 2023, Huu ni ukuaji mkubwa zaidi katika kipindi cha muda mfupi cha uongozi wa awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ndani ya miaka miwili pato hilo limeongezeka kwa Dola za Marekani Bilioni 16 (TZS trilioni 37.616) ikilinganishwa na ukuaji wa miaka sita ya awamu ya tano ambapo pato hilo lilikua kwa Dola za Marekani Bilioni 12 pekee (TZS trilioni 28.212). Vilevile IMF imeonesha kuwa kwa mwenendo uliopo hadi mwaka 2028 Tanzania kutakuwa na watu milioni 73.36 huku pato la Taifa likitarajiwa kukua hadi dola bilioni 136.09 (TZS trilioni 318.8) na pato la mtu mmoja mmoja likitarajiwa kukua hadi dola 1,860 (TZS milioni 4.3), huku kasi ya ukuaji wa uchumi ikitarajiwa kuwa asilimia 7. Ukuaji huu wa uchumi ni matokeo ya jitihada za makusudi za Mheshimiwa Rais ambapo tangu alipoingia madarakani Machi mwaka 2021, ametekeleza sera rafiki kwa sekta binafsi, ambayo imeongeza kasi ya uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi nchini huku akifungua fursa za ajira kwa wananchi kote nchini. Kazi hii kubwa ya ukuaji wa uchumi ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inaeleza lengo la kukuza kwa Pato la Taifa pamoja na kujenga uchumi wa kisasa, shirikishi na shindani, utakaowezesha ustawi wa wananchi. Read More