Mheshimiwa Rais aanzisha mageuzi yatakayoleta ufanisi kwenye mashirika ya umma

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameianzisha safari itakayoshuhudia mageuzi makubwa ya mashirika ya umma, taasisi na wakala za Serikali ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na kuziwezesha taasisi hizo kujiendesha kwa tija na ufanisi ili kupunguza utegemezo kutoka Serikalini.

Mageuzi hayo yametokana na uhalisia kuwa licha ya wingi wa mashirika na wakala hizo (248) ambazo Serikali imewekeza mtaji wa TZS trilioni 73, bado mchango wake kwenye uchumi ni mdogo sana, kwani kwa sasa taasisi hizo zinachangia asilimia 3 tu kwenye bajeti ya Serikali, huku nyingi zikitegemea ruzuku ili kujiendesha.

Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa maono ya Mwalimu Nyerere kuanzisha mashirika ya umma alitaka yamilikiwe na wananchi wenyewe kupitia hisa na kwamba wananchi washirikishwe kwenye masuala ya mashirika hayo, na hivyo ameagiza hatua zichukuliwe ili kurudi kwenye msingi huo. “Kwa kuwa kwa sasa wapo wananchi wenye uwezo wa kununua hisa, hata kama ni kidogo kidogo, nadhani turejee kwenye mwelekeo huo,” ameagiza.

Ili kufikia malengo hayo, Mheshimiwa Rais ameridhia mabadiliko mbalimbali ambayo ni pamoja na kutoa uhuru kwa taasisi kujiendesha katika mambo ya msingi, kufanya maboresho katika taratibu za ajira kwa watumishi wao na katika sheria ya ununuzi wa umma, na kuongeza kusiwepo kwa kuingiliwa kisiasa kwenye utendaji wa taasisi hizi.

Pia, Serikali ipo kwenye mchakato wa kutunga sheria itakayobadili hadhi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, na kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ili kuondoa utegemezi kutoka mfuko mkuu wa Serikali.

Kutokana na uchunguzi uliobaini uwepo wa taasisi ambazo majukumu yake yanashabihiana au hayana umuhimu kwa sasa na zile ambazo zinalega lega Serikali itaziunganisha au kutatua changamoto zao ziwezeshe kujiendesha kwani mashirika hayo ni muhimu kwa uchumi zikiwa zinatoa asilimia 17 ya ajira zote nchini. Amewatoa hofu watumishi kuwa mabadiliko yatakayofanyika hayataathiri ajira zao kwa namna yoyote ile.

“Mpango huu, tunaamini, utaipunguzia Serikali gharama za uendeshaji, na kuongeza ufanisi na tija ya utendaji,” amesema Rais Samia huku akitaka ushirikishwa kwa wadau wote kwenye mabadiliko haya ili kuepusha ukiukwaji wa sheria ambao unaweza kuleta hasara mbeleni.