Sera nzuri za uchumi za Rais Samia zaleta neema kwa mabenki

Sera nzuri za uchumi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimi wa Rais Samia Suluhu Hassan zimeendelea kuleta neema kubwa kwenye sekta ya benki nchini, moja ya uthibitisho huo ukiwa ni namna benki za kibiashara zinavyovunja rekodi ya mapato na faida mwaka.

Faida ya benki hizo ni ishara ya usimamizi imara wa sera ya fedha inayopelekea uchumi kuwa tulivu na kuwa moja ya uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani pamoja na kutanuka kwa huduma za kifedha zinazoendelea kuifnya Tanzania kusogea karibu zaidi na lengo la kuwa na huduma za kifedha jumuishi.

Taarifa za robo ya nne ya mwaka (Oktoba-Desemba 2023) za mabenki ambazo zimechapishwa Januari 2024 zinaonesha kuwa benki mbili kubwa nchini, CRDB na NMB, zinaendelea kuwa vinara wa sekta ya fedha nchini ambapo NMB imevunja rekodi kwa kupata faida ghafi shilingi bilioni 775.

Kutokana na mazingira mazuri ya uchumi nchini tangu Rais Samia aingie madarakani NMB imeongeza kiasi cha mikopo inayotoa kwa asilimia 28, hadi kufikia Shilingi trilioni 7.7 mwaka jana, hatua ambayo imewanufaisha maelfu ya wananchi, huku wengine wakinufaika kwa kuwa mawakala na kupata ajira kutokana na kupanuka kwa shughuli za benki hiyo.

Kwa upande wa CRDB imeongeza jumla ya mali (total assets) kufikia shilingi trilioni 13.2, amana za wateja (customer deposits) ziliongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 8.8 na mikopo inayotoa imeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 8.8.

Benki za biashara zinatarajiwa kuweka rekodi mpya ya faida mwaka huu mpya wa 2024 na kutoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi kutokana na mazingira mazuri ya uchumi na uwekezaji chini ya serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia.

Uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania kuanza kutekeleza Sera ya Fedha kwa kigezo cha riba ya mikopo kwenda benki za kibiashara kunatarajiwa kuinufaisha maradufu Tanzania kwa kuhakikisha ukwasi wa kutosha kwenye shughuli za kiuchumi na kupunguza mfumuko wa bei nchini.