Tanzania yaweka historia kununua hisa za kitalu gesi cha Mnazi Bay

Katika kitabu cha historia na rekodi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa taifa letu, leo amefungua sura mpya ambapo Tanzania kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa mara ya kwanza limeongeza hisa za umiliki na ushiriki kwenye kitalu cha gesi kwa kununua hisa asilimia 20 kati ya hisa asilimia 31.94 za kampuni ya WentWorth Resources katika kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay mkoani Mtwara.

Kufuatia hatua hiyo, umiliki wa Tanzania kwenye kitalu hicho umefikia asilimia 40, huku kampuni ya Maurel & Prom Tanzania ikinunua hisa asilimia 11.94, na hivyo kufikisha umiliki wa asilimia 60 wa kitalu hicho, na leo kampuni hizo mbili zimesaini mikataba miwili; wa kwanza wa mauziano ya hisa na wa pili wa uendeshaji wa kitalu cha gesi asilia cha Mnazi Bay

Hatua ya Tanzania kuongeza umiliki kwenye kitalu hicho ina manufaa mengi ikiwa ni pamona na kuongeza mapato ya Serikali, kuimarisha usalama wa upatikanaji wa nishati nchini, ikiwafahamika kuwa asilimia 65 ya umeme unaotumika nchini ni wa gesi asilia. Manufaa mengine ni kuepusha kitalu kumilikiwa na kuendeshwa na kampuni moja, pamoja na TPDC kuwa na nguvu katika uendeshaji na uendelezaji za kitalu hicho hatua itakayowajengea uwezo zaidi.

Kupitia mkataba mpya, sasa uamuzi wa uendeshaji na uendelezaji wa kitalu utafanywa na wanahisa wote, tofauti na awali ambapo Maurel & Prom ambayo ilikuwa inamiliki asilimia 48.05 ilikuwa ifanya shughuli hizo kwa niaba ya wanahisa wengine. Aidha, TPDC imepata haki ya kupeleka wafanyakazi katika shughuli za uendeshaji na uendelezaji kitalu kwa muda mrefu tofauti na awali ambapo walikuwa wanakwenda kwa muda mfupi tu, hivyo kutawajengea uwezo wataalamu wa ndani.

Mageuzi haya ya kihistoria yanayofanyika chini ya Mheshimiwa Rais Samia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (2020-2025) ambayo imeelekeza Serikali kutekeleza mapinduzi ya kiuchumi kwa maendeleo ya watu ambao ndio wanapaswa kuwa wanufaika wakuu wa rasilimali za nchi.

Aidha, Tanzania inajipanga kuongeza matumizi ya gesi, hasa majumbani, ikiwa lengo ni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033, huku lengo jingine likiwa ni kuiuza kwa nchi jirani za Zambia, Kenya, Uganda na DR Congo ambapo kwa nchi tatu za mwanzo tayari makubaliano yameshafikiwa.