Miradi ya Uwekezaji
-
Sera nzuri za uchumi za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu zimeendelea kuweka rekodi ambazo hazijawahi kufikiwa katika historia ya taifa letu ambapo shughuli kuu za kiuchumi za utalii, madini na uzalishaji viwandani zimeendelea kufanya vizuri zaidi. Mwaka 2023 mapato yatokanayo na utalii na dhahabu kwa mara ya kwanza yalivuka dola za Kimarekani bilioni 3 (zaidi ya TZS trilioni 7.6), huku uuzaji nje wa bidhaa za viwandani ukiendelea kuwa juu ya kiwango cha dola za Kimarekani bilioni 1 tangu MAMA aingie madarakani. Matokeo haya ambayo hayakuwahi kufikiwa kabla ni ushahidi kuwa sera nzuri za Rais Samia zinalipa ambapo kupaa kwa mapato ya utalii na dhahabu kumeiwezesha nchini kupunguza urari wa biashara kutoka TZS trilioni 13.6 mwaka 2022 hadi kufikia TZS trilioni 7.2 mwaka 2023. Takwimu toka Benki Kuu ya Tanzania zinaonesha kuwa shughuli mbalimbali za kiuchumi zimeimarika kuvuka kiwango kilichokuwepo kabla ya janga la UVIKO19, hali inayothibitisha kuwa, sio tu uchumi unaimarika kutoka kwenye janga hilo, bali unakuwa kwa kasi ambayo haijawahi kufikiwa kabla. Wakati sekta za kiuchumi zikiendelea kufanya vizuri, mfumuko wa bei umeendelea kushuka ambapo kwa wastani mwaka 2023 ulikuwa asilimia 3 kutoka asilimia 3.2 mwaka 2022, sawa na malengo ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Read More
-
Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai – Septemba) imeongezeka kufikia miradi 137 kutoka miradi 82 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 67. Aidha, ongezeko hilo limechochea pia kupata ongezeko maradufu la ajira zinazotokana na miradi ya uwekezaji kufikia ajira 86,986 ikilinganishwa na ajira 12,008 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2022/23, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 624. Matokeo ya kufurika kwa uwekezaji nchini Tanzania ni matunda ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuanzia kuwenye uboreshaji wa sheria, kanuni na taratibu, kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuimarisha amani na utulivu pamoja, matumizi ya TEHAMA na kurahisisha utoaji wa leseni na vibali. Pia, ziara za Mheshimiwa Rais Samia nje ya nchi zimechangia kuongezeka kwa uwekezaji nchini ambapo maeneo mengi anayokwenda amekuwa akiambatana na sekta binafsi ya Tanzania ambapo pia hukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa wa nchi anayokwenda, hivyo kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini, hatua inayowapelekea kuja kuwekeza nchini. Ongezeko hilo linafanya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa nchini kuanzia Januari hadi Septemba 2023 kufikia 366, sawa na asilimia 91.5 ya lengo la kusajili miradi 400 kwa mwaka huu. Miradi hiyo iliyosajiliwa hadi Septemba 2023 inatarajiwa kutoa ajira 116,986 pamoja na kuwekeza mtaji wenye thamani ya zaidi ya TZS trilioni 9.5 ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi. Lengo la Mheshimiwa Rais Samia na kuiwezesha Tanzania kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025. Read More
-
Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezeka kwa mwezi mmoja kufikia TZS trilioni 2.33 kwa Agosti mwaka huu kutoka TZS trilioni 1.06 kwa Julai mwaka huu, sawa na ukuaji wa asilimia 120. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji imeongezeka kufikia 58 kutoka 40 katika kipindi tajwa, ambapo kwa miradi iliyosajiliwa Agosti mwaka huu inatarajiwa kuzalisha ajira 25,700. Ongezeko la miradi limeendelea kusadifu mikakati na mkazo uliowekwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kilimo ili kuboresha maisha ya Watanzania ikizangatiwa sekta hii kwa takwimu za mwaka 2021 ilichangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, ilitoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Matokeo ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais imeendelea kuonekana ambapo thamani ya uwekezaji kwenye kilimo imeongezeka kwa zaidi ya TZS bilioni 275.53 kufikia TZS bilioni 849.13 kutoka TZS bilioni 571.1 kwa Julai mwaka huu. Wakati uwekezaji kwenye kilimo ukiendele kukua, Serikali imeendelea kuchua hatua kumwezesha mkulima mdogo ikiwemo kuimarisha huduma za ugani, kutoa ruzuku na pembejeo za kilimo, kufungua fursa za masoko, kujenga mifumo ya umwagiliaji, kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, hasa kwa vijana, pamoja na afua nyingine ili kuwezesha kilimo kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2030. Wanazuoni wamepongeza mageuzi yanayoendelea kufanyika kwenye kilimo ambapo Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kuwekeza zaidi kwenye kilimo, huku Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja amesema Tanzania inatambulika duniani kwa fursa nyingi kwenye kilimo. Read More
-
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi ya uwekezaji 229 yenye thamani ya TZS trilioni 4.5 kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, ambapo lengo ni kufikia miradi 400 ifikapo Desemba 2023. Idadi hiyo inadhihirisha kasi kubwa ya usajili wa miradi nchini ikilinganishwa na miradi 293 iliyosajiliwa mwaka 2022, hivyo kusajili asilimia 78 ya miradi hiyo ndani ya nusu mwaka ni mafanikio makubwa kwa nchi. Kusajiliwa kwa miradi hiyo inayotoa ajira zaidi ya 30,000 kwa Watanzania katika sekta mbalimbali ni matokeo ya sera ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ikiwemo kuboresha sheria, kupunguza tozo/kodi mbalimbali na kuimarisha amani na utulivu. Aidha, takwimu zinaonesha mkakati huo wa Rais umefanikiwa zaidi kwani kwa miaka sita ya Serikali ya awamu ya tano, jumla ya miradi ya TZS trilioni 45 ilisajiliwa, huku miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita ikisajili miradi ya trilioni 22 ndani ya miaka miwili, takwimu zinazoonesha kuwa itafanya vizuri kuliko awamu iliyopita. Aidha, sababu nyingine ni taasisi 12 za usimamizi kuwa katika jengo moja hivyo kurahisisha utoaji huduma pamoja na matumizi ya TEHAMA yaliyorahisisha utoaji wa leseni na vibali mbalimbali vya biashara na uwekezaji hasa kupitia dirisha ya kielektroniki ambapo mwekezaji sasa anaweza kuwasilisha maombi akiwa popote dunia Read More
-
Tanzania imevutia uwekezaji wa TZS trilioni 2.8 katika kipindi cha miezi mitatu (Januari – Machi 2023) kutokana na mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanzania kuwa eneo bora la biashara na uwekezaji. Takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) za Machi 2023 zinaonesha kuwa kutokana na miradi 93 iliyosajiliwa katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/23, Watanzania watanufaika na fursa za ajira zaidi ya 16,400. Idadi hiyo ya uwekezaji ni ukuaji wa asilimia 48.9 ikilinganishwa na miradi ya uwekezaji wa TZS trilioni 1.8 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2022. Aidha, ni ongezeko la asilimia 160 ikilinganishwa na uwekezaji wa TZS trilioni 1.1 uliosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021. Kwa miradi 37 iliyosajiliwa Machi 2023 pekee, nusu inamilikiwa na wazawa, huku wageni na ubia ikiwa ni asilimia 31 na asilimia 19 mtawala, hali inayoashiria kukua kwa uchumi na mazingira bora ya uwekezaji. Ziara ya Rais Samia nchini Afrika Kusini na ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris nchini Tanzania imetoa fursa ya kutangaza fursa za uwekezaji, ambapo kati ya kampuni 12 za Afrika Kusini zilizoonesha utayari wa kuwekezaji nchini, tayari moja imekuja kuangalia fursa za uwekezaji. Uamuzi wa Tanzania kurejea kwenye taasisi za kimataifa za usuluhishi pia umechangia kuongeza wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa huduma za usafirishaji, pamoja na ufanisi wa bandari. Read More
-
Mkakati wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuboresha mazingira ya biashara nchini na kuvutia uwakezaji umezaa matunda ambapo takwimu kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa thamani ya uwekezaji nchini umekua kwa asilimia 173. Ripoti ya TIC inaonesha kuwa thamani ya uwekezaji imepanda kufikia TZS trilioni 19.87 katika miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita, kutoka TZS trilioni 7.27 iliyorekodiwa katika miaka miwili kabla hajaingia madarakani. Ongezeko hilo ni matokeo ya kazi kubwa ya Rais ya kurejesha imani ya wawekezaji ndani na nje ya nchi ambao amekuwa akikutana katika ziara zake nje ya nchi na ndani ya nchi ambapo pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji, pia alizipatia ufumbuzi changamoto zilizowakabili. Kati ya Machi 2021 na Februari 2023 idadi ya miradi iliyosajiliwa imeongezeka kutoka 455 hadi 575, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 26. Kati ya miradi hiyo, asilimia 32 inamilikiwa na Watanzania, asilimia 42 ni ya wageni na asilimi 27 ni ubia kati ya wageni na wazawa. Kutokana na uwekezaji huo, idadi ya ajira zilizozalishwa kwa Watanzania zimeongezeka kutoka 61,900 hadi 87,187, uwekezaji mkubwa ukiwa kwenye sekta za viwanda, ujenzi wa majengo ya kibiashara na usafirishaji. Mafanikio haya yamehusishwa pia na Tanzania kushiriki katika mikutano ya kimataifa. Read More
-
Kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika nchini kwa kuboresha mazingira ya biashara kupitia mabadiliko ya kisheria na kanuni, ujenzi wa miundombinu na uainishaji maeneo muhimu kwa uwekezaji na biashara, uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2023 unatarajiwa kukua kwa asilimia 5 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022. Akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ambapo kwa kipindi kifupi cha Julai hadi Novemba kilishuhudia ongezeko la asilimia 22 la miradi iliyosajiliwa nchini kwa kipindi hicho kufikia miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 ambayo itatoa ajira 21,297. “Mabadiliko mbalimbali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Blueprint) yamechochea ukuaji wa sekta binafsi na kurejesha nguvu ya soko na kupunguza mwingilio wa serikali katika shughuli za kiuchumi, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa uwekezaji nchini,” amesema Rais Samia. Mkakati wa Rais Samia wa kuimarisha sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa kunawezesha kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa vijana wengi kujiajiri na kuajiri kupitia sekta hiyo, kwani takribani vijana milioni 1 huingia kwenye soko la ajira nchini kila mwaka, idadi ambayo Serikali pekee haiwezi kuwahudumia. Kupitia ujenzi wa miradi ya kimkakati unaoendelea nchini ikiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), reli ya kisasa, ujenzi na ukarabati wa meli mbalimbali, bomba la mafuta (EACOP) na mradi wa kuchakata gesi asilia mkoani Lindi, anaamini kuwa uchumi wa Tanzania utaendelea kuimarika na kuwanufaisha Watanzania zaidi. Wakati huo huo, amesema ana imani kuwa kila Mtanzania anayo nafasi katika maendeleo na mustakabali wa Tanzania na kuwa wananchi wanahaki na uhuru ambao wanastahili kuufurahia kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo nchini. Read More