Kitaifa

  • Mageuzi ya Mama Yanaendelea: Benki Kuu yatangaza sera mpya ya fedha

    Moja ya falsafa za uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ni Mageuzi (Reforms) ambapo mwaka 2023 yalifanyika makubwa ikiwemo kuanzisha wizara mpya, mageuzi ndani ya wizara, kuanzishwa kwa Tume ya Mipango pamoja na mitaala ya elimu. Mageuzi hayo yanaendelea mwaka 2024 ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuanzia Januari 2024 itaanza kutumia mfumo unaotumia riba katika kutekeleza Sera ya Fedha, badala ya mfumo unaotumia ujazi wa fedha, mabadiliko ambayo yanalenga kuongeza ufanisi wa sera ya fedha katika kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha shughuli za kiuchumi. Awali BoT katika utekelezaji wa Sera ya Fedha (kusimamia uchumi, mfumuko wa bei, mzunguko wa fedha, thamani ya shilingi na ustawi wa sekta ya fedha) ilifanya hivyo kwa kutumia kiwango cha fedha kilichopo mtaani (kwenye mzunguko), ambapo ilipunguza fedha kwenye mzunguko au kuziongeza kutokana na hali ya wakati huo, mfano mfumuko wa bei. Katika mfumo mpya wa kutumia riba, ambayo itafahamika kama Riba ya Benki Kuu (CBR), BoT itatekeleza majukumu yake kwa kupandisha au kushusha kiwango cha riba kwa mikopo kwenda benki za kibiashara, ili kuongeza au kupunguza fedha kwenye mzunguko au kukabiliana na changamoto nyingine ya kiuchumi kwa wakati husika. Kwa kutumia mfumo wa CBR, benki kuu inatekeleza makubaliano ya kutumia mfumo mmoja wa utekelezaji wa sera ya fedha katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za kiuchumi ambazo Tanzania ni mwanachama. Mbali na kuhakikisha ukwasi katika uchumi, kukuza uchumi na kudhibiti mfumuko wa bei, riba hiyo itatumika pia kama kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini. Hii ikimaanisha kuwa, kadiri riba ya BoT itakavyozidi kuwa ndogo, kutatoa uwezekano mkubwa kwa wananchi kupata mikopo kwa riba nafuu zaidi. Hata hivyo, BoT imesisitiza kuwa riba yake haimaanishi kuweka ukomo katika viwango vya riba zinazotozwa na benki na taasisi nyingine za fedha… Read More

  • MAMA ni mwanamageuzi: Maboresho ya sheria yaongeza uwezo wa wazawa kuwekeza nchin

    Mtaji wa uwekezaji ya wazawa umefikia wastani wa asilimia 50 ya miradi yote iliyosajiliwa kila mwezi, ikiwa ni matokeo ya mwaka mmoja tu baada ya serikali kupunguza kiwango cha mtaji wa uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani, kutoka dola za Kimarekani 100,000 (shilingi milioni 250) hadi dola za Kimarekani 50,000 (Shilingi milioni 125). Mafanikio hayo chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ni matokeo ya maboresho ya Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya mwaka 2022 ambayo imeweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji, mifumo ya kitaasisi, ulinzi, vivutio, kutoa motisha na kurahisisha uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) miradi ya uwekezaji wa ndani ilichangia wastani wa asilimia 20 ya miradi yote kabla ya kutekelezwa kwa sheria mpya ambapo mwaka 2021 Tanzania ilikuwa na miradi yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 2 bilioni iliyosajiliwa, lakini kwa mwezi Agosti pekee mwaka huu, Tanzania imesajili miradi yenye thamani ya takribani dola za Kimarekani bilioni 1. Ongezeko la uwekezaji wa ndani linatoa matumaini mapya nchini kwa kuimarisha sekta binafsi, kupunguza changamoto za ajira na kuongeza ushawishi kwa wa ushirikiano na kampuni za nje zinazohitaji ubia na kampuni za ndani zenye uhakika wa mtaji. Aidha, sheria hiyo inatoa ahueni kubwa zaidi kwa wawekezaji wazawa kwani endapo hana fedha inayofikia kiwango husika, lakini thamani ya mali aliyonayo, mfano shamba, mashine au malighafi nyingine ambazo zinafikia thamani hiyo anaweza kusajiliwa na TIC na kunufaika na vivutio vya uwekezaji.   Read More

  • Mheshimiwa Rais Samia afungua fursa ya ajira 500 kwa wauguzi Saudi Arabia

    Katika kuendelea kufungua fursa za ajira ndani na nje ya nchi, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imetangaza neema ya uwepo wa ajira 500 za wauguzi wa kike kuajiriwa na Serikali ya Saudi Arabia mapema Januari 2024. Ajira hizo ni matokeo ya Mheshimiwa Rais Samia kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani, ambapo mwishoni mwa Novemba na mwanzoni wa Desemba 2023 Tanzania imesaini hati mbili za makubaliano ya ushirikiano katika masuala ya kazi na ajira na Saudi Arabia pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu. Hati hizo zinatoa fursa za ajira kwenye mataifa husika kwa kada na sekta zenye kutumia ujuzi wa chini, ujuzi wa kati na ujuzi wa juu na pia zinaweka utaratibu rasmi wa kuratibu ajira za Watanzania wanaoenda kufanya kazi nje, ili kuhakikisha wajibu na haki za zao zinalindwa na kuzingatiwa ipasavyo. Alisema watanzania wote wenye sifa na ujuzi uliobainishwa wanataarifiwa kuomba kazi husika kwa kujisajili https://jobs.kazi.go.tz na kutuma wasifu binafsi (CV) kwa njia ya barua pepe esu@taesa.go.tz, ambapo mwisho wa kutuma maombi ni Desemba 27, 2024. Wakati huo huo, Serikali inaendelea kufanya mashauriano katika hatua mbalimbali na nchi nyingine zaidi ya 10 kwa lengo la kuwa na makubaliano ya ushirikiano utakaowezesha Watanzania kunufaika na fursa za ajira kwenye nchi husika. Read More

  • Tanzania yatenga hekta 63,000 za uwekezaji mkubwa wa kilimo na ufugaji

    Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imetenga eneo lenye rutuba la ukubwa wa hekta 60,103 kwaajili ya mji wa kilimo (kilimo kikubwa cha kibiashara pamoja na ufugaji wa kisasa) litakalotolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Eneo hilo lipo Mkulazi mkoani Morogoro, pembezoni mwa reli ya TAZARA na linafaa kwaajili ya kilimo cha miwa, mpunga, mahindi, mtama na mengineyo. Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inakusudia kupunguza uagizaji wa mazao kutoka nje, pamoja na kuwa kapu la chakula la kulisha nchi nyingine. Kilimo cha miwa kitaongeza malighafi kwenye viwanda vya uzalishaji wa sukari na hivyo kuiwezesha nchi kuachana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Tanzania iliagiza tani 30,000 za sukari ili kufidia nakisi ya uzalishaji wa ndani. Mashamba manne (kila moja likiwa na ukubwa wa hekta 10,000) zitatumiwa kwa ajili kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na aina ya udongo, shamba jingine lenye ukubwa wa hekta 10,000 litatengwa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na usindikaji wa mazao ya mifugo, huku hekta 10,103 zilizobaki zikihifadhiwa kwa matumizi ya baadaye kwa ajili ya kuanzisha maeneo ya usindikaji wa bidhaa za kilimo na viwanda vya kuongezea thamani bidhaa za kilimo. Katika hatua nyingine ya kuvutia uwekezaji, TIC imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 3,200 mkoani Kigoma kwa ajili kilimo cha michikichi, usindikaji wa mawese na kilimo cha mazao mengine. Hatua hii pia itaiwezesha nchi kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula ambapo kwa takwimu za sasa 60% ya bidhaa hiyo muhimu inatoka nje ya nchi ikiigharimu nchi zaidi ya TZS bilioni 627 kwa mwaka. Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa Tanzania imetumia 33% tu ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo, hivyo kuwa na fursa kubwa ya kujikuza kupitia kilimo cha kibiashara, ambapo sasa serikali imeweka mkakati wa kuifungua. Read More

  • Mheshimiwa Rais Samia akatisha ziara Dubai ili kushughulikia mafuriko Hanang

    Kutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara na kupelekea vifo vya zaidi ya watu 50, kujeruhi wengine zaidi ya 80 pamoja na kuharibu makazi ya watu na mali mbalimbali, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amekatisha ziara yake iliyokuwa inaendelea Dubai. Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Dubai kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) amekatisha safari hiyo na anarejea nchini ili kushughulikia kwa karibu janga hilo. Aidha, ametoa maelekezo kuwa serikali igharamie mazishi ya wote waliofariki na majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama viendelea kutoa msaada wa dharura na uokoaji. Pia, ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao. Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza tathmini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida. Ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba mkubwa uliowakumba na pia amewahakikishia wananchi walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao na itahakikisha inashughulikia masuala yote yaliotokana na janga hili. Read More

  • Mheshimiwa Rais Samia alivyoipa kipaumbele sekta binafsi kwenye mageuzi ya kilimo nchini

    Tanzania imeweka mkakati wa kutumia mageuzi ya kilimo kupunguza umaskini wa wananchi ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo. Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Usalama wa Chakula, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema Tanzania imekuja na Ajenda ya 10/30 ambayo inalenga kuwezesha kilimo kukua kwa asilimia 10, kutoka asilimia 4 ya sasa, ifikapo mwaka 2030. Mheshimiwa Rais ametaja hatua ambazo Serikali imechukua na inaendelea kuchukua ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio vya kikodi kwa sekta binafsi ili ishiriki kikamilifu kwenye kilimo. Vivutio hivyo ni pamoja na kutoa punguzo la kodi (capital allowance) kwa asilimia 100, kusamehe ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani katika vifaa vya kilimo ikiwemo vya vifaa vitakavyotumika katika umwagiliaji, uongezaji thamani, kulima na nishati salama, hatua ambayo inalenga kupunguza gharama za uwekezaji. Hatua nyingine ni Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kufanya kilimo cha kisasa, mradi ambao utawezesha kuongeza uzalishaji na kutunza mazingira. “Kutunza mazingira bila kupunguza umaskini tutakuwa tunafanya kazi bure,” amesema huku akiongeza kuwa kazi ya Serikali ni kuwapa vijana mafunzo na ardhi, hivyo sasa sekta binafsi inatakiwa iingie kwenye kutoa fedha, lakini pia mitambo kufanya kilimo chetu kiwe cha kisasa Pia, amebainisha kuwa mkazo umewekwa katika tafiti ili kuwezesha wananchi kufanya kilimo chenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, ukame, wadudu na kutunza mazingira. Katika eneo hili Serikali imejenga na inahamasisha sekta binafsi kujenga skimu za umwagiliaji na mabwawa ya kuvuna maji ya mvua. “Sekta binafsi itakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaongeza thamani mazao yote yanayozalishwa, lakini pia biashara ya kilimo,” amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza kuwa katika hili Serikali inahakikisha upatikanaji wa ardhi na utoaji wa leseni na vibali kwa wawekezaji wanaotaka kuingia kwenye kilimo cha… Read More

  • Mama Ameifungua Nchi: Miradi ya uwekezaji yaongezeka zaidi ya mara mbili

    Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 (Julai – Septemba) imeongezeka kufikia miradi 137 kutoka miradi 82 kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 67. Aidha, ongezeko hilo limechochea pia kupata ongezeko maradufu la ajira zinazotokana na miradi ya uwekezaji kufikia ajira 86,986 ikilinganishwa na ajira 12,008 zilizopatikana kipindi kama hicho mwaka 2022/23, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 624. Matokeo ya kufurika kwa uwekezaji nchini Tanzania ni matunda ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa kuanzia kuwenye uboreshaji wa sheria, kanuni na taratibu, kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuimarisha amani na utulivu pamoja, matumizi ya TEHAMA na kurahisisha utoaji wa leseni na vibali. Pia, ziara za Mheshimiwa Rais Samia nje ya nchi zimechangia kuongezeka kwa uwekezaji nchini ambapo maeneo mengi anayokwenda amekuwa akiambatana na sekta binafsi ya Tanzania ambapo pia hukutana na kuzungumza na wafanyabiashara wakubwa wa nchi anayokwenda, hivyo kuwaeleza fursa za uwekezaji nchini, hatua inayowapelekea kuja kuwekeza nchini. Ongezeko hilo linafanya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa nchini kuanzia Januari hadi Septemba 2023 kufikia 366, sawa na asilimia 91.5 ya lengo la kusajili miradi 400 kwa mwaka huu. Miradi hiyo iliyosajiliwa hadi Septemba 2023 inatarajiwa kutoa ajira 116,986 pamoja na kuwekeza mtaji wenye thamani ya zaidi ya TZS trilioni 9.5 ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi. Lengo la Mheshimiwa Rais Samia na kuiwezesha Tanzania kusajili miradi ya uwekezaji kutoka nje (FDI) yenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 15 (TZS trilioni 37.5) ifikapo mwaka 2025. Read More

  • Mheshimiwa Rais Samia aweka historia mageuzi sheria za uchaguzi

    Julai 1 mwaka jana wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 30 ya demokrasia, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu katika barua yake ya wazi aliandika, “Serikali yangu itajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria zetu za uchaguzi […] Mabadiliko katika sheria zetu za uchaguzi, yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza.” Mwaka mmoja baadaye, Serikali yake imeonesha dhamira ya kutekeleza hilo ambapo imewasilisha bungeni miswada mitatu, Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa, yote ya mwaka 2023. Miongoni mwa mabadiliko yanayotarajiwa kutokana miswada hiyo ni kuifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa huru zaidi kwa kujitegemea ambapo itaajiri watumishi wake yenyewe, badala ya utaratibu wa sasa wa kuazima watumishi kutoka taasisi nyingine. Aidha, wajumbe watano wa NEC watateuliwa baada ya kutuma maombi na kufanyiwa usaili na Kamati ya Usaili, hatua inayoongeza uwazi ikiwa ni utekelezaji wa maoni ya wadau. Pia, Serikali inakusudia kuunganisha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292, ili kuwezesha uchaguzi mkuu kusimamiwa na sheria moja, tofauti na sasa ambapo uchaguzi wa madiwani unasimamiwa na sheria ya serikali za mitaa. Uwepo wa sheria moja utaondoa mkanganyiko kwa wadau wa uchaguzi, hususan vyama vya siasa na waangalizi wa uchaguzi. Kwa upande wa vyama vya siasa, muswada umeweka mkazo katika kuzingatiwa kwa jinsia na makundi maalum katika vipaumbele vya vyama na shughuli za kisiasa. Maboresho mengine ni kudhibiti kauli zinazochochea vurugu na vitendo vya ukatili wa kijinsia. Aidha, muswada wa uchaguzi unakusudia kuondoa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa, ambapo sasa nafasi ya Rais, Mbunge au Diwani ikiwa na mgombea mmoja, atapigiwa kura na atatangazwa kuwa mshindi endapo kura za NDIO zitazidi… Read More

  • Mageuzi sekta ya elimu: Mitaala mipya kuzalisha wahitimu wanaoweza kujiajiri

    Agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan la kuboresha mfumo wa elimu ili kumwezesha muhitimu kujiajiri na kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake limefanyiwa kazi ambapo serikali imekamilisha uandaaji na uidhinishaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na mitaala katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na mafunzo ya ualimu kwa lengo la kufanya elimu inayotolewa iendane na wakati. Kama alivyoelekeza Mheshimiwa Rais Samia, mitaala iliyoboreshwa imezingatia mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo katika stadi za karne ya 21 ili kumjengea mhitimu stadi za kuwasiliana, kushirikiana, ubunifu na fikra tunduizi. Aidha, kwa upande wa elimu ya kati na elimu ya juu, mapitio ya programu mbalimbali pia yanaendelea kwa lengo la kuifanya iendane na wakati, vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira ambapo elimu ya juu programu zaidi ya 300 zitahuishwa au kuanzishwa. Uamuzi huo wa kimageuzi wa Mheshimiwa Rais umetokana na uhalisia kwamba mfumo wa elimu wa sasa umejikita zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo, mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu na upungufu wa nguvu kazi. Kwa maboresho hayo ambayo yataanza kutekelezwa mwaka 2027, elimu ya lazima itakuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa, ambapo mtihani wa darasa la saba utafutwa na badala yake kuanza kufanyika kwa tathimini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari. Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya msingi na sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana, pia itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali. Read More

  • Diplomasia ya Uchumi: Mheshimiwa Rais Samia aivuta Zambia kutumia zaidi Bandari ya Dar es Salaam

    Katika kuendelea kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji hasa kutoka nje ya Tanzania kutumia Bandari ya Dar es Salaam kupitisha mizigo yao, Serikali ya Tanzania imetenga hekta 20 za ardhi katika Bandari Kavu ya Kwala mkoani Pwani kwa ajili ya mizigo inayokwenda Zambia, ikiwa ni sehemu ya kurahisisha ufanyaji biashara. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa Zambia katika Bandari ya Dar es Salaam, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa mizigo inayokwenda nchini humo itakuwa na kipindi cha neema (bure) kirefu zaidi cha kuhifadhi mizigo yao hadi siku 45, ikiwa ni mkakati wa kupunguza msongamano na ucheleweshaji, na hivyo kupunguza gharama za biashara. Mheshimiwa Rais Samia alisema hayo akihutubia katika maadhimisho ya miaka 59 ya uhuru wa Zambia ambapo alikuwa mgeni rasmi, na kuongeza kuwa “tunatarajia kuwa hatua hii itaongeza biashara kati ya nchi zetu mbili na kuzalisha fursa zaidi kwa ajili ya wananchi wetu. Hii ni zawadi kutoka kwa Tanzania mkisherehekea uhuru wenu.” Zambia ni nchi ye pili kwa kupitisha shehena kubwa ya mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam baada ya DR Congo ambapo kwa mwaka 2022 ilipitisha tani milioni 1.98, sawa na asilimia 24 ya mizigo yote iliyokwenda nje. Aidha, ifahamike kuwa asilimia 80 ya mizigo yote inayopita bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi, inapita katika mpaka wa Zambia, jambo linaloifanya nchi hiyo kuwa mshirika wa kimkakati. Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Samia umekuja wakati ambapo Tanzania imeanza mageuzi ya kiutendaji katika Bandari Dar es Salaam yatakayowezesha kupokea meli kubwa zaidi na kutoa huduma kwa kasi, hivyo inaihitaji sana Zambia kuwa na imani na mazingira mazuri ya biashara ili iendelee kuitumia bandari hiyo, badala ya kugeukia bandari shindani. Mbali na bandari, Mheshimiwa Rais Samia ameeleza azma ya Serikali yake kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika ukanda wa kusini na ukanda wa mashariki ili kuongeza usambazaji wa umeme… Read More