Mafanikio makubwa ya kiuchumi robo ya kwanza mwaka 2024 yamedhihirisha maono ya MAMA

Utekelezaji imara wa sera za kiuchumi, kuimarika kwa amani na utulivu na mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuifungua nchi kumeendelea kuimarisha uchumi wa Tanzania licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa dunia, uimara unaotarajiwa kuendelea katika siku zijazo, hususan robo ya pili ya mwaka 2024.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeainisha maeneo matano ambayo yameendelea kudhihirisha kuimarika kwa uchumi wa Tanzania katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 ambapo kwanza ni ukuaji wa uchumi unakadiriwa kufikia asilimia 5.1 ikiwa ni matokeo ya uwekezaji unaofanywa na Serikali kuongeza uwekezaji kwa sekta binafsi.

Ripoti ya BoT imeeleza kuwa hatua zinazochukuliwa na Mheshimiwa Rais Samia zinachangia kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji kutoka nje ya nchi. Mikopo hiyo ambayo inatarajiwa kuendelea kuongezeka ilielekezwa zaidi katika shughuli za kilimo, uchimbaji wa madini, usafirishaji na uzalishaji viwandani sawasawa na malengo ya Serikali.

Eneo jingine ni mfumuko wa bei ambao umeendelea kuwa tulivu, kwa wastani wa asilimia 3, hali inayotokana na utekelezaji wa sera madhubuti ya fedha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini, hivyo kuifanya Tanzania moja ya nchi chache zenye kiwango kidogo cha mfumuko wa bei Afrika. Kiwango hicho kipo ndani ya lengo la nchi la mfumuko wa bei usiozidi asilimia 5 na vigezo vya kikanda kwa jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama.

Matokeo ya uwekezaji na uzalishaji yameendelea kuzaa matunda ambapo nakisi ya urari wa biashara nje ya nchi iliendelea kupungua kutokana na kupungua kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na kuongezeka kwa mauzo nje ya nchi. Nakisi imepungua kwa zaidi ya asilimia 50, kufikia dola milioni 2,701.4 mwaka unaoishi Februari 2024, kutoka dola milioni 5,133.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Kuongezeka kwa mauzo nje kumechangia kuongeza akiba ya fedha za kigeni ambapo imeendelea kuwa ya kutosha, kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 5.3 mwishoni mwa Machi 2024, sawa na miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.

Wakati huo huo, kuimarika kwa biashara na uwekezaji kumeimarisha utekelezaji wa sera ya bajeti ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 mapato ya Serikali yalikuwa takribani asilimia 95 ya lengo kwa Tanzania Bara.

Mafanikio haya, ambayo ni sehemu tu ya makubwa aliyoyafanya MAMA katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ni uthibitisho wa namna sera zake zinakuza uchumi hasa kwa kuimarisha sekta ambazo zinagusa maisha ya mamilioni ya watanzania ikiwemo kilimo, madini na uzalishaji viwandani.