Maeneo 8 ya vipaumbele ya Mheshimiwa Rais Samia uandaaji wa Dira ya 2050

Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa dira mpya ya Taifa ya maendeleo ya miaka 25 (mwaka 2025 hadi mwaka 2050) ambayo itakuwa ni dira ya pili kuandaliwa nchini baada ya ile iliyoanza mwaka 2000 na inatarajiwa kumalizika mwaka 2025.

Akizindua mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi kwa ajili ya kuandaa dira mpya, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameainisha maeneo nane ya kipaumbele katika dira mpya ambayo yanatokana na mahitaji ya sasa ya dunia, makosa na mafanikio yaliyotokana na utekelezaji wa dira inatoelekea ukomo pamoja na mahitaji mengine ya kitaifa.

Kwanza, ukuaji wa uchumi kufungamanishwa na sekta za uzalishaji zinazowagusa wananchi wengi zaidi na kutengeneza ajira kwaajili yao kama vile sekta ya kilimo. Pili, kukusanywa kwa takwimu kutoka sekta isiyo rasmi ili kupata hali halisi ya uchumi badala ya kutumia takwimu za sekta rasmi pekee, hali inayosababisha kukosa uhalisia wa hali ya uchumi.

Eneo la tatu ni tathmini na ufuatiliaji ambao utawezesha kubaini viashiria vya kasoro kwenye utekelezaji wa dira mapema na kuzifanyia kazi ili kuhakikisha malengo yanafikiwa. Nne, uratibu wa kufungamanisha miradi ya kipaumbele kwa sekta zinazohusika katika uzalishaji. Katika hili Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa mipango ya sekta moja inapotekelezwa iwe na mwingiliano na mchango katika sekta nyingine ili kutumia rasilimali chache kwa matokeo makubwa.

Tano, amesisitiza dira iweke mwelekeo wa uwekezaji na usimamizi wa maboresho ya kiutendaji wa mashirika ya serikali ili yaongeze ufanisi katika uendeshaji na yaweze kuhimili ushindani wa kikanda na kimataifa. Ushiriki wa sekta binafsi katika kukuza uchumi ni eneo la sita alilolitaja ambapo amesema lazima sekta binafsi iimarishwe na iwe tayari kuimarika ili ziwe na uwezo na utayari wa kufanya biashara, kutengeneza ajira pamoja na kushirikiana na sekta binafsi nje ya nchi. Uimarishaji huo unajumuisha uwepo wa mifumo rafiki ya kisheria, upatikanaji wa mitaji na rasilimali watu yenye ujuzi.

Kuzingatiwa kwa maadili ya Taifa ni sehemu ya saba ya kuzingatia katika uandaaji wa dira. Ameeleza licha ya kuwa Serikali imepiga hatua katika kusimamia maadili kwenye utumishi wa umma, lakini hiyo haitoshi kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania wapo nje ya mfumo wa utumishi wa umma, hivyo kama nchi lazima iwe na misingi ambayo itazingatiwa kwa uzito mkubwa. Misingi itakayozalisha watu jasiri, wapinga rushwa, wapenda haki, mahiri, makini na waadilifu.

Eneo la nane ni kubaini viashiria vya mambo yanayoweza kuathiri Taifa, wananchi na utekelezaji wa dira ya Taifa kama vile matishio ya kimazingira, vita, mabadiliko ya teknolojia, ongezeko la bei ya mafuta na uhaba wa dola, matukio ya dharura yanayoweza kuibuka duniani au nchini, na kubaini namna ya kudhibiti hathari zake. Amesisitiza kuwa ni lazima kuwe na mbinu za kujihami na kujenga uhimilivu wa jamii.

Katika kufanya haya yote, Mheshimiwa Rais Samia amesisitiza ushirikishwaji wa makundi yote kwenye jamii na kuzingatiwa hali na uwezo wa nchi.