Uwekezaji Tanzania
-
Kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika nchini kwa kuboresha mazingira ya biashara kupitia mabadiliko ya kisheria na kanuni, ujenzi wa miundombinu na uainishaji maeneo muhimu kwa uwekezaji na biashara, uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2023 unatarajiwa kukua kwa asilimia 5 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022. Akizungumza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi (Diplomatic Sherry Party), Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema mwaka 2022 ulikuwa mwaka wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ambapo kwa kipindi kifupi cha Julai hadi Novemba kilishuhudia ongezeko la asilimia 22 la miradi iliyosajiliwa nchini kwa kipindi hicho kufikia miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 ambayo itatoa ajira 21,297. “Mabadiliko mbalimbali kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (Blueprint) yamechochea ukuaji wa sekta binafsi na kurejesha nguvu ya soko na kupunguza mwingilio wa serikali katika shughuli za kiuchumi, jambo ambalo limepelekea kuongezeka kwa uwekezaji nchini,” amesema Rais Samia. Mkakati wa Rais Samia wa kuimarisha sekta binafsi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa kunawezesha kupunguza tatizo la ajira nchini, kwa vijana wengi kujiajiri na kuajiri kupitia sekta hiyo, kwani takribani vijana milioni 1 huingia kwenye soko la ajira nchini kila mwaka, idadi ambayo Serikali pekee haiwezi kuwahudumia. Kupitia ujenzi wa miradi ya kimkakati unaoendelea nchini ikiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), reli ya kisasa, ujenzi na ukarabati wa meli mbalimbali, bomba la mafuta (EACOP) na mradi wa kuchakata gesi asilia mkoani Lindi, anaamini kuwa uchumi wa Tanzania utaendelea kuimarika na kuwanufaisha Watanzania zaidi. Wakati huo huo, amesema ana imani kuwa kila Mtanzania anayo nafasi katika maendeleo na mustakabali wa Tanzania na kuwa wananchi wanahaki na uhuru ambao wanastahili kuufurahia kwa mujibu wa kanuni na sheria zilizopo nchini. Read More
-
Mkakati wa kibiashara wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan unaendelea kuwa na matokeo chanya katika dira ya Serikali ya kukuza uchumi ambapo takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezaka karibu mara tatu ndani ya kipindi cha miezi mitano. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimetoa taarifa inayoonesha kuwa kimesajili miradi 132 yenye thamani ya TZS trilioni 7 kati ya Julai hadi Novemba mwaka huu ambapo sekta ya viwanda, usafirishaji na utalii ndizo zimeongoza kwa uwekezaji. Usajili huo ni ongezeko la miradi 24 kutoka miradi 108 yenye thamani ya TZS trilioni 2.06 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka 2021. Miradi hiyo ambayo imeongezeka kwa idadi na thamani, itatoa ajira 21,297 ambazo ni ongezeko la asilimia 57 kutoka ajira 13,578 za mwaka jana ni matokeo ya Diplomasia ya Uchumi ambayo Rais amekuwa akiitekeleza kwa vitendo. Rais Samia ameendelea kuimarisha mahusiano ya kibiashara ndani ya nchi, kikanda na kimataifa katika ziara mbalimbali anazofanya ambazo huambatana na wafanyabiashara wa ndani ambao hupata fursa ya kuzungumza na wafanyabiashara wa nje, lakini pia huwezesha Tanzania na nchi nyingine kuingia makubaliano ya kibiashara na uwekezaji. Tangu aingie madarakani Rais amefanikiwa kurejesha imani ya wawekezaji ambao sasa wanaamani ya kuja na kuwekeza nchini. Katika muda huo ametatua changamoto mbalimbali za kibiashara kama vile kupunguza muda wa kupata vibali vya uwekezaji, kurekebisha mifumo ya kikodi, kuondoa ukiritimba wa vibali vya kazi na kuwepo kwa maeneo maalum ya uwekezaji. Read More