Ukuaji wa Uchumi
-
Ripoti ya uchumi ya robo ya pili imethibitisha kuwa hatua za kimkakati zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zinaleta matokeo yanayowezesha uchumi kustahimili na kukua licha ya changamoto za janga UVIKO19, vita ya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi. Katika kipindi hicho (Aprili-Juni 2023) ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonesha kuwa uchumi umekua kwa asilimia 5.2, ikiwa ni hatua kubwa kutoka asilimia 4.7 na asilimia 3.8 zilizorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2022 na mwaka 2021, mtawalia. Shuguli zote za kiuchumi zilizofanyika katika kipindi hicho zimechangia katika ukuaji huo, lakini sekta iliyokuwa na mchango mkubwa zaidi kilimo (11.9%), hali inayoonesha mwitikio mkubwa wa mkazo ambao Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameuweka kwenye kilimo. Sekta nyingine ni usafiri na utunzaji mizigo (11.6%), fedha na bima (10.5%), biashara na ukarabati (10.3%), viwanda (9.2%) na ujenzi 6.9%). Aidha, sekta za kiuchumi zilizoshuhudia ukuaji mkubwa ni huduma za kifedha na bima (15.6%), umeme (12.4%), huduma nyinginezo zinazojumuisha sanaa, burudani na shughuli za majumbani (11.5%) usafiri na uhifadhi mizigo (7.6%), chakula na malazi (7.2%), biashara na ukarabati (7.6%) pamoja na madini (6.3%). Ukuaji huo unalandana na takwimu za ripoti ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) iliyotolewa Oktoba 2023 ambayo imeonesha kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.2 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022, huku ukuaji kwa mwaka 2023 ukitarajiwa kufikia asilimia 6.1. Takwimu za IMF zinaifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi 10 za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unatazamiwa kukua kwa kasi. Read More
-
Licha ya kuwa ukuaji wa bara la Afrika unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 4.1 mwaka 2022 hadi asilimia 3.8 mwaka 2023, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua zaidi huku Umoja wa Mataifa (UN) ukiitaja kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi mwaka 2023. Tanzania ambayo inaendelea kuwa mfano Afrika kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, inatarajiwa kushuhudia ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.6, ikitanguliwa na Ivory Coast ambayo uchumi wake utakua kwa asilimia 6.5 pamoja na Rwanda itakayoshuhudia ukuaji wa asilimia 7.8. Mafanikio hayo ni matokeo ya mikakati ya Rais Samia ambapo katika miaka miwili ya uongozi wake amesajili miradi ya uwekezaji ya TZS trilioni 17, ambayo imechochea ukuaji wa sekta nyingine pamoja na kutoa fursa za ajira kwa maelfu ya Watanzania. Mikakati hiyo pia imewezesha uchumi kukabiliana na changamoto za dunia kama mfumuko wa bei, gharama kubwa za ukopaji na mabadiliko ya tabianchi. Wakati ripoti ya UN ikionesha hivyo, Benki ya Dunia (WB) imeitaja Tanzania kuwa nchi ya 10 kwa utajiri barani Afrika kwa kwa kuzingatia Pato Ghafi la Taifa (FDP) kwa kuangalia viwango vya sasa vya kubadili fedha. Ukuaji huo mbali na kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania lakini pia unawapa imani wawekezaji waliopo na wanaokusudia kuwekeza nchini, kwa kuwafanya waamini Tanzania ni sehemu salama kuwekeza mitaji yao ya mabilioni, hivyo kufanya uchumi kukua zaidi na zaidi. Read More
-
Ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Pato la Ghafi la Taifa (GDP) limekua kutoka TZS trilioni 163.3 mwaka 2021 hadi TZS trilioni 200, sawa na ukuaji wa asilimia 23. Takwimu hizo za Shirika la Fedha Duniani (IMF) zinadhihirisha matokeo chanya ya mkakati wa Rais wa kuifungua nchi na kukaribisha wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na kufufua biashara za ndani ambazo zilikuwa zimefungwa. Kwa ukuaji huo, ni dhahiri kuwa uchumi wa Tanzania sasa ni mkubwa kuliko baadhi ya nchi za Ulaya kama Croatia, Lithunia, Serbia na Slovenia, hatua ambayo imerejesha imani ya wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini. Tanzania sasa inashika nafasi ya 6 kati ya nchi 10 za Kusini mwa Jangwa la Sahara zenye uchumi mkubwa zaidi, ikitanguliwa na Nigeria, Afrika Kusini, Ethiopia, Kenya na Angola. Aidha, kwa mujibu wa IMF, uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kufikia TZS trilioni 318 ifikapo mwaka 2028, ukuaji ambapo utaakisi uwezo wa Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na huduma za kijamii. Read More