Mama hana jambo dogo: Uchumi wakua kwa asilimia 5.2 robo ya pili ya mwaka 2023

Ripoti ya uchumi ya robo ya pili imethibitisha kuwa hatua za kimkakati zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zinaleta matokeo yanayowezesha uchumi kustahimili na kukua licha ya changamoto za janga UVIKO19, vita ya Urusi na Ukraine na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kipindi hicho (Aprili-Juni 2023) ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imeonesha kuwa uchumi umekua kwa asilimia 5.2, ikiwa ni hatua kubwa kutoka asilimia 4.7 na asilimia 3.8 zilizorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2022 na mwaka 2021, mtawalia.

Shuguli zote za kiuchumi zilizofanyika katika kipindi hicho zimechangia katika ukuaji huo, lakini sekta iliyokuwa na mchango mkubwa zaidi kilimo (11.9%), hali inayoonesha mwitikio mkubwa wa mkazo ambao Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameuweka kwenye kilimo. Sekta nyingine ni usafiri na utunzaji mizigo (11.6%), fedha na bima (10.5%), biashara na ukarabati (10.3%), viwanda (9.2%) na ujenzi 6.9%).

Aidha, sekta za kiuchumi zilizoshuhudia ukuaji mkubwa ni huduma za kifedha na bima (15.6%), umeme (12.4%), huduma nyinginezo zinazojumuisha sanaa, burudani na shughuli za majumbani (11.5%) usafiri na uhifadhi mizigo (7.6%), chakula na malazi (7.2%), biashara na ukarabati (7.6%) pamoja na madini (6.3%).

Ukuaji huo unalandana na takwimu za ripoti ya Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) iliyotolewa Oktoba 2023 ambayo imeonesha kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.2 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022, huku ukuaji kwa mwaka 2023 ukitarajiwa kufikia asilimia 6.1.

Takwimu za IMF zinaifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi 10 za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unatazamiwa kukua kwa kasi.