Pembejeo za Kilimo

  • Tanzania yatenga hekta 63,000 za uwekezaji mkubwa wa kilimo na ufugaji

    Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imetenga eneo lenye rutuba la ukubwa wa hekta 60,103 kwaajili ya mji wa kilimo (kilimo kikubwa cha kibiashara pamoja na ufugaji wa kisasa) litakalotolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Eneo hilo lipo Mkulazi mkoani Morogoro, pembezoni mwa reli ya TAZARA na linafaa kwaajili ya kilimo cha miwa, mpunga, mahindi, mtama na mengineyo. Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inakusudia kupunguza uagizaji wa mazao kutoka nje, pamoja na kuwa kapu la chakula la kulisha nchi nyingine. Kilimo cha miwa kitaongeza malighafi kwenye viwanda vya uzalishaji wa sukari na hivyo kuiwezesha nchi kuachana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Tanzania iliagiza tani 30,000 za sukari ili kufidia nakisi ya uzalishaji wa ndani. Mashamba manne (kila moja likiwa na ukubwa wa hekta 10,000) zitatumiwa kwa ajili kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na aina ya udongo, shamba jingine lenye ukubwa wa hekta 10,000 litatengwa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na usindikaji wa mazao ya mifugo, huku hekta 10,103 zilizobaki zikihifadhiwa kwa matumizi ya baadaye kwa ajili ya kuanzisha maeneo ya usindikaji wa bidhaa za kilimo na viwanda vya kuongezea thamani bidhaa za kilimo. Katika hatua nyingine ya kuvutia uwekezaji, TIC imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 3,200 mkoani Kigoma kwa ajili kilimo cha michikichi, usindikaji wa mawese na kilimo cha mazao mengine. Hatua hii pia itaiwezesha nchi kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula ambapo kwa takwimu za sasa 60% ya bidhaa hiyo muhimu inatoka nje ya nchi ikiigharimu nchi zaidi ya TZS bilioni 627 kwa mwaka. Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa Tanzania imetumia 33% tu ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo, hivyo kuwa na fursa kubwa ya kujikuza kupitia kilimo cha kibiashara, ambapo sasa serikali imeweka mkakati wa kuifungua. Read More

  • #MiakaMiwiliYaMama: Amewajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia kilimo

    Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anadhihirisha kwa vitendo kauli yake aliyotoa kuwa hataki kuingia katika historia ya kuwa mmoja wa wanaowalaumu vijana kuwa hawajiajiri, badala yake anawawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri kupitia kilimo ambapo lengo ni kuzalisha ajira milioni 3, kipaumbele kikiwa vijana na wanawake. Machi 20 mwaka huu amezindua mashamba ya pamoja (Block Farms) zaidi ya ekari 12,000 ambazo zitagawawiwa kwa vijana, kila mmoja kwa ukubwa usiozidi ekari 10, pia alizindua ndege zisizo na rubani, mashine za umwagiliaji na magari kwa ajili ya maafisa wa wilaya ili kuhakikisha vijana popote walipo nchini wanapata usaidizi wa kitaalamu katika kufanya kilimo cha kibiashara. Katika azma ya kukifanya kilimo kuwa cha vijana, ameahidi kuendelea kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya watendaji kwenye sekta ya kilimo ili shughuli zote zifanyike kwa usasa kuanzia uzalishaji hadi uuzaji mazao na bidhaa. “Tunasema ni kilimo cha vijana, hivyo vijana wawepo shambani, wawepo kwenye utaalamu, wawepo kwenye kuendesha mitambao, sehemu zote kuwa na vijana wanaokwenda kwenye sekta ya kilimo,” amesema akizindua programu ya Building a Better Tomorrow. Katika miaka miwili ya uongozi wake, kilimo ni moja tu ya njia anazotumia kumwinua kijana wa Kitanzania na kukabiliana na changamoto ya ajira inayoisumbua dunia. Ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya, mikopo ya halmashauri, kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa wajasiriamali ni maeneo mengine ambayo yametoa ajira kwa vijana wengi. Read More

  • #MiakaMiwiliYaMama: Fursa zaidi kwa vijana, sasa Serikali kuwapatia pembejeo za kilimo

    Katika moja ya hotuba zake kwa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere alieleza umuhimu wa kubadili mfumo wa kilimo nchini akisema kuwa kilimo cha kutegemea mvua, kisicho na mbolea, dawa na maarifa, hakitusaidii sana. Anayoyafanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) ni kuyaishi maono ya Mwalimu Nyerere kwani anakuza kilimo kwa kuwapatia vijana pembejeo (dawa, mbegu bora, viuatilifu), ili kubadili kilimo na kufikia lengo la kumnufaisha mkulima, kukuza mchango wake kwenye uchumi, kuongeza uzalishaji wa chakula na malighafi za viwandani. Kama hilo halitoshi, Machi 20 mwaka huu Rais atazindua programu ya Building a Better Tomorrow – Youth Agribusiness Initiative (BBT-YIA) ambapo katika awamu ya kwanza vijana 812 watapatiwa mafunzo kwa miezi minne bure, kisha watapewa mashamba ambayo tayari yamewekewa mifumo ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo. Ikiwa kati ya Watanzania 10, saba wanajishughulisha na kilimo, na ikiwa vijana ndio nguvu kazi kubwa, uamuzi wa Rais kuwekeza kwa vijana kwenye kilimo utabadili dhana kuwa kilimo hakilipi, kilimo ni cha wazee na changamoto ya ajira ambayo inawakabili vijana duniani kote itapungua nchini. Rais ametoa wito wa sekta binafsi na taasisi za kimataifa kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha vijana na wanawake, hasa kuwapatia mitaji ya shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji ili kuwawezesha kufikia malengo binafsi na ya kitaifa. Read More