#MiakaMiwiliYaMama: Amewajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia kilimo

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anadhihirisha kwa vitendo kauli yake aliyotoa kuwa hataki kuingia katika historia ya kuwa mmoja wa wanaowalaumu vijana kuwa hawajiajiri, badala yake anawawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri kupitia kilimo ambapo lengo ni kuzalisha ajira milioni 3, kipaumbele kikiwa vijana na wanawake.

Machi 20 mwaka huu amezindua mashamba ya pamoja (Block Farms) zaidi ya ekari 12,000 ambazo zitagawawiwa kwa vijana, kila mmoja kwa ukubwa usiozidi ekari 10, pia alizindua ndege zisizo na rubani, mashine za umwagiliaji na magari kwa ajili ya maafisa wa wilaya ili kuhakikisha vijana popote walipo nchini wanapata usaidizi wa kitaalamu katika kufanya kilimo cha kibiashara.

Katika azma ya kukifanya kilimo kuwa cha vijana, ameahidi kuendelea kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya watendaji kwenye sekta ya kilimo ili shughuli zote zifanyike kwa usasa kuanzia uzalishaji hadi uuzaji mazao na bidhaa.

“Tunasema ni kilimo cha vijana, hivyo vijana wawepo shambani, wawepo kwenye utaalamu, wawepo kwenye kuendesha mitambao, sehemu zote kuwa na vijana wanaokwenda kwenye sekta ya kilimo,” amesema akizindua programu ya Building a Better Tomorrow.

Katika miaka miwili ya uongozi wake, kilimo ni moja tu ya njia anazotumia kumwinua kijana wa Kitanzania na kukabiliana na changamoto ya ajira inayoisumbua dunia. Ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika kila wilaya, mikopo ya halmashauri, kuboresha mazingira ya biashara hasa kwa wajasiriamali ni maeneo mengine ambayo yametoa ajira kwa vijana wengi.