Uwekezaj Tanzania
-
Mei mwaka huu Tanzania ilivunja rekodi iliyodumu kwa miaka 10 kwa kusajili miradi mpya ya uwekezaji 52 yenye thamani ya TZS bilioni 783, ikitarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 6,200 ikiwa ni matokeo ya sera za kibiashara za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia ameifungua nchi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini hatua ambayo imerejesha imani ya wawekezaji ambao wameiona Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza mabilioni yao ya mitaji pamoja na kuvutia uwekezaji mpya. Kutokana na mkakati huo mwamko wa wakezaji wa ndani nao umekuwa mkubwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza ambapo kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) asilimia 50 iliyosajiliwa kati ya Aprili hadi Juni mwaka huu inamilikiwa na wazawa, mingine ikiwa ni ya wageni na ubia, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 20 iliyokuwepo Januari. Ongezeko la uwekezaji nchini limeendelea kuwa na manufaa kwa Watanzania ambapo zaidi ya ajira za moja kwa moja 30,000 zinatokana na miradi yote iliyosajiliwa kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, huku kukiwa na maelfu ya fursa za ajira zisizo za moja kwa moja. Manufaa mengine ni kuchochea ukuaji wa uchumi, pia kuongezeka kwa uwekezaji kunajenga imani kwa wawekezaji wapya kuja nchini. Katika kurahisisha biashara na uwekezaji, Serikali imeanzisha kituo cha pamoja ambacho kina jumla ya taasisi 12 zinazohusika na sekta hiyo ambacho kinarahisisha utoaji wa leseni, vibali na nyaraka nyingine muhimu ndani ya muda mfupi. Aidha, Mei mwaka huu TIC imeanza kutumia mfumo wa Dirisha la Pamoja la Kuhudumia Wawekezaji la Kielektroniki Tanzania (TeIW) ambalo limekuwa suluhisho katika kurahisha upokeaji wa maombi, utoaji wa huduma za vibali, leseni na usajili kwa wawekezaji kwa haraka. Lengo la Mfumo huo ni kutumika kurahisisha mtiririko wa taarifa kati ya taasisi zote zilizoko ndani ya kituo. Read More