Rasilimali Watu Afrika

  • Tanzania ni ya mfano Afrika kwa uwekezaji katika rasilimali watu

    Wakuu wa nchi za Afrika, viongozi wa ngazi mbalimbali na wadau wengine wamekusanyika Tanzania kujadili mustakabali wa rasilimali watu barani Afrika ambapo Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu ametumia jukwaa hilo kueleza hatua mbalimbali ambazo Tanzania imezichukua kuimarisha sekta hiyo ambayo ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya afua mbalimbali za lishe na huduma za afya ya uzazi wa mama na mtoto. Hatua nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na elimu ili kuondoa udumavu ambao, mara nyingi, hupunguza kiwango cha uelewa na uwezo wa kusoma kwa waoto na kuhakikisha watoto wanaandaliwa kimwili, kiakili, kiisimu/kijinsia kiubunifu na kiakili-hisia. Aidha, Serikali imetoa afua kwa kaya masikini, inatoa elimu bila malipo kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita, inapanua elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, imefuta ada kwa baadhi ya vyuo vya ufundi, imeanza kutoa mikopo kwa vyuo vya kati, inatoa mikopo kwa vijana, inaruhusu waliokatisha masomo kurejea shule pamoja na kuweka mkakati wa kuvutia vijana kwenye kilimo, yote haya yakilenga kuongeza mchango wao kwenye uchumi. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022, vijana ndio kundi lenye watu wengi zaidi nchini Tanzania, hivyo hatua ambazo Rais ameeleza kuwa Tanzania imezichukua kwa asilimia kubwa zimewalenga vijana kwani anaamini kwamba maisha bora ambayo vijana wengi hukimbilia Ulaya kuyafuata yanaweza kupatikana barani Afrika endapo Serikali zao zitawawezesha. “Viongozi wenye maono hujenga sera zao kwenye maendeleo ya watu na kufuatiwa na maendeleo ya vitu,” amesema Rais Samia akitoa wito kwa viongozi wenzake wa Afrika na kusisitiza kwamba Afrika haitoweza kuendelea endapo rasilimali watu isipoendelezwa. Read More