Rais Samia Suluhu

  • Benki ya Dunia yataja miujiza mitano uchumi wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu

    Benki ya Dunia (WB) imeipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi hali inayoonekana kama miujiza wakati huu ambapo chumi za nchi mbalimbali duniani zinadorora kutokana na athari za janga la UVIKO19, vita ya Urusi na Ukraine, kupanda kwa bei ya mafuta na mabadiliko ya tabianchi. Akitoa pongezi hizo, Makamu Rais wa Benki ya Dunia wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwaka amesema kuwa wakati nchi mbalimbali zikihangaika na janga la mfumuko wa bei wa tarakimu mbili, huku akiitaja Ghana kuwa na mfumuko wa bei wa 30%, Tanzania imeweza kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu moja tu, ambapo kwa Septemba ulikuwa 4.8%. Athari za kuwa na mfumuko mkubwa wa bei ni kuwa kunapandisha bei za bidhaa, kunapunguza uwezo wa kufanya manunuzi, hivyo kuathiri hali ya maisha ya wananchi. “Tumeona karibu nchi nyingi duniani zikiwa na akiba ndogo ya fedha za kigeni, lakini Tanzania imeweza kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi mitano,” amesema Kwaka. Fedha za kigeni zinaiwezesha serikali kutimiza mahitaji yake ya fedha za kigeni na mahitaji ya kuagiza bidhaa kutoka nje, kutoa imani kwamba serikali inaweza ikatimiza majukumu yake ya muda mfupi kulipa madeni ya nje na kusaidia utekelezaji wa sera za fedha na kubadilisha fedha za kigeni, pamoja na uwezo wa kuingilia kuhakikisha fedha ya taifa ni imara. Kuhusu nakisi ya bajeti amesema mataifa mataifa mengi yakihangaika kwa kuwa na nakisi kubwa ya bajeti, Tanzania ina nakisi ndogo ya 3.5% ya Pato la Taifa. Nakisi ndogo ya bajeti kwanza ni ishara nzuri kuwa uchumi wa Taifa unaimarika na ina maana kuwa nchi itahitaji kukopa kiasi kidogo cha fedha au kutokuweka kodi kubwa ili kupata fedha za kufadhili bajeti yake. Kwaka pia ameipongeza Tanzania kwa kuwa na sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye… Read More

  • Historia, Rais Samia akizima majenereta na kuwasha umeme wa gridi ya Taifa Kigoma

    Rais Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 17, 2022 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi amewasha umeme wa Gridi ya Taifa katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma na kuzima mitambo mitatu ya mafuta yenye iliyokuwa ikizalisha umeme megawati 3.75 zilizotumika Wilaya ya Kasulu na Buhigwe. Uzimaji wa majenereta wilayani Kasulu ni mwendelezo wa uzimaji majenerata katika maeneo mbalimbali baada ya umeme wa gridi ya Taifa, ambapo maeneo mengine ni Kibondo, Loliondo, Ngara na Biharamulo. Kwa kuendesha majenereta kwa mkoa wa Kigoma pekee, Serikali ilikuwa ikipata hasara ya TZS bilioni 36 kila mwaka, kwani gharama za uendeshaji majenereta ilikuwa TZS bilioni 52 huku mapato yakiwa TZS bilioni 14. Mbali na kuondoa hasara hiyo umeme wa gridi ya Taifa utawezesha wakazi wa Kigoma kupata umeme wa kutosha ambapo uhitaji ni megawati 14, na Serikali imepeka megawati 20. Aidha, umeme utachochea shughuli za kiuchumi na uwekezaji katika sekta za biashara, viwanda, madini na kilimo, hivyo kuongeza mapato ya wananchi na Taifa. Pia, umeme utaimarisha shughuli za ulinzi na usalama na utoaji huduma zakijamii kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine. Read More

  • Rais Samia aidhinisha bilioni 160 kujenga madarasa 8,000

    Jumla ya wanafunzi 1,384,340 wamefanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka 2021. Wanafunzi wao ni zao la kwanza mpango wa elimu bila ada ulioanza mwaka 2016, ulioshuhudia idadi kubwa ya watoto wakiandikishwa darasa la kwanza. Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha TZS bilioni 160 ambazo zitatumika kujenga madarasa 8,000 kwenye shule za sekondari 2,439 zilizoainishwa kuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa nchini. Madarasa hayo yatakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 400,000 ambao ni sehemu ya wanafunzi 1,148,512 wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023. Idadi ya wanafunzi wanaobaki watatumia vyumba vya madarasa vilivyoachwa na wanafunzi 422,403 waliohitimu kidato cha nne mwaka huu, pamoja na madarasa katika shule mpya za kata 231 zilizojengwa. Katika salamu za heri kwa watahiniwa hao Rais amewaahidi kuwa “Serikali itahakikisha maandalizi ya miundombinu ya kuwapokea wote watakaoendelea na kidato cha kwanza mwakani 2023 inakamilika.” Mwaka 2021 aliweka historia kwa kuwezesha wanafunzi wote waliofaulu kidato cha kwanza kuanza masomo kwa wakati mmoja baada ya kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000, hivyo kuweka mazingira rafiki ya ufundishaji na watoto wote kupata muda sawa masomo. Kwa hatua hii, Rais Samia anatekeleza matakwa ya ibara ya 11(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoitaka Serikali kufanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vinginevyo vya mafunzo. Read More