Mashirika ya Umma
-
Moja ya ‘R’ katika falasafa ya 4R ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inawakilisha’Reforms’ (Mabadiliko) ambapo amelenga kutoa fursa zaidi kwa watu wengi zaidi kunufaika kiuchumi badala ya wachache. Matokeo ya mabadiliko hayo kiuchumi tunaendelea kuyashuhudia ambapo mabadiliko yaliyofanywa kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma umeongeza gawio linalotolewa kwa Serikali kwa mwaka 2024/25. Gawio hilo limeongeza kwa asilimia 40 toka TZS bilioni 633.3 mwaka 2023/24 hadi zaidi ya TZS bilioni 900 iliyokusanywa hadi sasa ambapo lengo ni kukusanya TZS trilioni 1 kabla ya Juni 10 mwaka huu ambapo gawio hilo litakabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais. Aidha, mabadiliko hayo si tu yameongeza gawio bali pia yameongeza mashirika yanayotoa gawio ambapo kwa mwaka huu ni zaidi ya 200 ikilinganishwa na wastani wa mashirika 146 kuanzia mwaka 2021/22 hadi mwaka 2023/24. Mageuzi yaliyofanywa ikiwemo kuyapa uhuru na kuyawezesha kujiendesha kibiashara yamewezesha mashirika yaliyokuwa yanapata hasara kuanza kupata faida. Mageuzi mengine ni kuunganishwa kwa taasisi 14 na kufutwa kwa taasisi nyingine, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na ufanisi katika kutathmini bodi za wakurugenzi. Haya ni mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kwani yanaipunguzia serikali mzigo wa kuhudumia taasisi hizo kwa kuzipa ruzuku, lakini pia kunaleta tija ya kuanzishwa kwa taasisi hizo hasa katika kuwahudumia wananchi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Read More
-
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameianzisha safari itakayoshuhudia mageuzi makubwa ya mashirika ya umma, taasisi na wakala za Serikali ikiwa ni utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na kuziwezesha taasisi hizo kujiendesha kwa tija na ufanisi ili kupunguza utegemezo kutoka Serikalini. Mageuzi hayo yametokana na uhalisia kuwa licha ya wingi wa mashirika na wakala hizo (248) ambazo Serikali imewekeza mtaji wa TZS trilioni 73, bado mchango wake kwenye uchumi ni mdogo sana, kwani kwa sasa taasisi hizo zinachangia asilimia 3 tu kwenye bajeti ya Serikali, huku nyingi zikitegemea ruzuku ili kujiendesha. Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa maono ya Mwalimu Nyerere kuanzisha mashirika ya umma alitaka yamilikiwe na wananchi wenyewe kupitia hisa na kwamba wananchi washirikishwe kwenye masuala ya mashirika hayo, na hivyo ameagiza hatua zichukuliwe ili kurudi kwenye msingi huo. “Kwa kuwa kwa sasa wapo wananchi wenye uwezo wa kununua hisa, hata kama ni kidogo kidogo, nadhani turejee kwenye mwelekeo huo,” ameagiza. Ili kufikia malengo hayo, Mheshimiwa Rais ameridhia mabadiliko mbalimbali ambayo ni pamoja na kutoa uhuru kwa taasisi kujiendesha katika mambo ya msingi, kufanya maboresho katika taratibu za ajira kwa watumishi wao na katika sheria ya ununuzi wa umma, na kuongeza kusiwepo kwa kuingiliwa kisiasa kwenye utendaji wa taasisi hizi. Pia, Serikali ipo kwenye mchakato wa kutunga sheria itakayobadili hadhi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, na kuangalia uwezekano wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma ili kuondoa utegemezi kutoka mfuko mkuu wa Serikali. Kutokana na uchunguzi uliobaini uwepo wa taasisi ambazo majukumu yake yanashabihiana au hayana umuhimu kwa sasa na zile ambazo zinalega lega Serikali itaziunganisha au kutatua changamoto zao ziwezeshe kujiendesha kwani mashirika hayo ni muhimu kwa uchumi zikiwa zinatoa asilimia 17 ya ajira zote nchini. Amewatoa hofu watumishi kuwa mabadiliko yatakayofanyika hayataathiri ajira zao… Read More
-
Katika kutelekeza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa mashirika na taasisi nyingine za Serikali au zile ambazo Serikali ina hisa nyingi zinajiendesha kwa faida, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechua ameainisha hatua tano za kimkakati ambazo zitachochea mabadiliko katika ufanisi wa taasisi hizo. Kwanza amesema ni kujenga utamaduni wa kukutana katika kikao kazi kila mwaka na watendaji na wenyeviti wa taasisi hizo. Pili, ni mabadiliko ya sheria ambayo yatahusisha kuondoa sheria zilizopitwa na wakati au zinazokwamisha mashirika kujiendesha kwa ufanisi. Hatua ya tatu ni kuangalia namna ya kuwapata viongozi wa kuendesha taasisi hizo ili kuhakikisha kuwa wanaopewa dhamana ni wenye ujuzi stahiki ambapo Mheshimiwa Rais amewahi kupendekeza kuwa nafasi hizo ziwe zinatangazwa, ili watu wenye sifa watume maombi. Nne ni uboresha wa bodi za taasisi hizo kwa kuangalia namna zinavyoteuliwa ambapo amesema lengo ni kuchagua watu wenye uwezo wa kiutendaji na kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. Hatua ya tano ni kutoa uhuru kwa taasisi hizo kuajiri ambapo mchakato huo tayari umeanza na kwa hatua ya kwanza wanaanza na taasisi za kibiashara na vyuo vikuu. Mchechu amesema baada ya hatua hizi, hatua zaidi za kimabadiliko zitachukuliwa ndani ya taasisi moja moja na viongozi husika na kuwa lengo ni kuziwezesha kuwa na ufanisi, kuongeza faida na kutoa gawio serikalini ili kupunguza utegemezi wa ruzuku. Read More