Mambo ya Nje Tanzania

  • ZAMA MPYA: Diaspora sasa kushiriki shughuli za kiuchumi na kijamii kidijitali

    Mchango wa Watanzania waishio nje ya nchi na wale wenye asili ya Tanzania katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi umeendelea kukua mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2022 waliwekeza nchini TZS bilioni 2.5 kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja. Aidha, takwimu za Benki ya Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha kuwa Diaspora ambao hadi sasa ni milioni 1.5, mwaka 2021 walituma nchini TZS trilioni 1.3, huku kiwango hicho kikiongezeka mara mbili mwaka 2022 kufikia TZS trilioni 2.6. Kutokana na nafasi yao hii jalili katika ustawi wa jamii na maendeleo, Serikali imeandaa mfumo wa kidijitali wa kuwasajili Diaspora wenye asili ya Tanzania (Diaspora Digital Hub) utakaoiwezesha kupata taarifa zao na wao kupata taarifa muhimu kutoka nchini. Mfumo huo wa aina yake utawezesha Serikali kupata taarifa sahihi za Diaspora kama vile jinsia, elimu na utaalamu na kuwawezesha Diaspora kushiriki kidijitali katika shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo wataweza kupata huduma za kibenki, hifadhi ya jamii, fursa za uwekezaji, biashara na masoko, masuala ya uhamiaji, vitambulisho vya taifa na huduma nyingine ambazo watazifikia kiurahisi. Diaspora wamekuwa wakichangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia biashara ya mali zisizohamishika (real estate) ambapo mwaka 2021 walinunua nyumba na viwanja vyenye thamani ya TZS bilioni 2.3 huku mwaka 2022 ununuzi huo ukipanda hadi TZS bilioni 4.4. Read More