Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania imetenga eneo lenye rutuba la ukubwa wa hekta 60,103 kwaajili ya mji wa kilimo (kilimo kikubwa cha kibiashara pamoja na ufugaji wa kisasa) litakalotolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Eneo hilo lipo Mkulazi mkoani Morogoro, pembezoni mwa reli ya TAZARA na linafaa kwaajili ya kilimo cha miwa, mpunga, mahindi, mtama na mengineyo. Kupitia uwekezaji huo, Tanzania inakusudia kupunguza uagizaji wa mazao kutoka nje, pamoja na kuwa kapu la chakula la kulisha nchi nyingine.
Kilimo cha miwa kitaongeza malighafi kwenye viwanda vya uzalishaji wa sukari na hivyo kuiwezesha nchi kuachana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje. Katika kipindi cha mwaka 2021/22 Tanzania iliagiza tani 30,000 za sukari ili kufidia nakisi ya uzalishaji wa ndani.
Mashamba manne (kila moja likiwa na ukubwa wa hekta 10,000) zitatumiwa kwa ajili kilimo cha mazao mbalimbali kulingana na aina ya udongo, shamba jingine lenye ukubwa wa hekta 10,000 litatengwa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa na usindikaji wa mazao ya mifugo, huku hekta 10,103 zilizobaki zikihifadhiwa kwa matumizi ya baadaye kwa ajili ya kuanzisha maeneo ya usindikaji wa bidhaa za kilimo na viwanda vya kuongezea thamani bidhaa za kilimo.
Katika hatua nyingine ya kuvutia uwekezaji, TIC imetenga eneo lenye ukubwa wa hekta 3,200 mkoani Kigoma kwa ajili kilimo cha michikichi, usindikaji wa mawese na kilimo cha mazao mengine. Hatua hii pia itaiwezesha nchi kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula ambapo kwa takwimu za sasa 60% ya bidhaa hiyo muhimu inatoka nje ya nchi ikiigharimu nchi zaidi ya TZS bilioni 627 kwa mwaka.
Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa Tanzania imetumia 33% tu ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo, hivyo kuwa na fursa kubwa ya kujikuza kupitia kilimo cha kibiashara, ambapo sasa serikali imeweka mkakati wa kuifungua.