Kutokana na mafuriko yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara na kupelekea vifo vya zaidi ya watu 50, kujeruhi wengine zaidi ya 80 pamoja na kuharibu makazi ya watu na mali mbalimbali, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amekatisha ziara yake iliyokuwa inaendelea Dubai.
Mheshimiwa Rais ambaye alikuwa Dubai kushiriki Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) amekatisha safari hiyo na anarejea nchini ili kushughulikia kwa karibu janga hilo.
Aidha, ametoa maelekezo kuwa serikali igharamie mazishi ya wote waliofariki na majeruhi wote ambao wapo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama viendelea kutoa msaada wa dharura na uokoaji.
Pia, ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia ameelekeza tathmini ya kina ifanyike juu ya maafa hayo na vitengo na taasisi zote za Serikali zinazohusika kuwepo eneo la tukio na kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali inarejea kawaida.
Ametoa pole kwa wafiwa wote kutokana na msiba mkubwa uliowakumba na pia amewahakikishia wananchi walioathirika kuwa serikali iko pamoja nao na itahakikisha inashughulikia masuala yote yaliotokana na janga hili.