Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Septemba 17, 2023 amemaliza ziara yake siku nne mkoani Mtwara, ziara ambayo imekuwa na mafanikio makubwa ikiendelea kuifungua Mtwara kuwa kitovu cha biashara kwa ajili ya Kanda ya Kusini pamoja na nchi jirani za Msumbiji, Malawi na Comoro.
Wakati wote wa ziara hiyo Mheshimiwa Rais alikagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumzia na wananchi, ambapo walieleza changamoto kubwa nne ambazo ni suala la maji, umeme, bei za mazao pamoja na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
Katika mkutano wake wa mwisho wilayani Masasi, ameeleza mkakati wa Serikali kutatua changamoto hizo ambazo kwa upande wa maji amesema kuwa kwa sasa mkoani Mtwara kuna miradi 66 inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ambayo inanufaisha vijiji 190, hivyo kufanya jumla ya vijiji vyenye majisafi na salama kufikia 650 kati ya vijiji takribani 750.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na uchimbaji wa visima, ikiwemo wilayani Liwale ambapo mitambo ya kuchimba visima ilianza kazi saa 24 baada ya Rais kumtaka waziri wa maji kuhakikisha changamoto ya wananchi hao inatatuliwa.
Kuhusu changamoto ya umeme, Mheshimiwa Rais amewaahidi wakazi wa mkoa huo baada ya miezi 18 changamoto hiyo itakuwa imekwisha kwa sababu miradi miwili mikubwa inatekeleza. Mradi wa kwanza ni wa kuunganisha Masasi kwenye gridi ya Taifa kwa kutoa umeme mkoani Ruvuma, na mradi wa pili ni kutoa umeme wilayani Ruangwa.
Aidha, kwa upande wa bei za mazao, amesema mkakati wa Serikali umewezesha mazao ya ufuta na mbaazi kupata bei nzuri msimu huu na kwamba anaamini korosho nayo itauzwa kwa bei nzuri. Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kuwa miaka miwili ijayo korosho yote utabanguliwa nchi kabla ya kusafirishwa, mkakati ambao utawanufaisha wakulima zaidi kwa kupandisha thamani zao hilo pamoja na ajira kwenye kongani ya viwanda ambayo itajengwa katika Kijiji cha Maranje wilayani Nanyumbu.
Mageuzi makubwa yanaendelea kwenye upande wa miundombinu ambapo sambamba na upanuzi wa uwanja wa ndege na Mtwara, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Masasi-Mnivata-Newala-Masasi ambapo kilomita 50 tayari zimekamilika na kilimota 160 zilizobaki tayari wakandarasi wawili wanaanza ujenzi ili kurahisisha usafiri na usafirishaji.
Aidha, mradi mwingine unaotarajiwa kutekelezwa ni ujenzi wa barabara ya Masasi-Nachingwea-Liwale (175km) ambapo ameahidi kila mwaka watatenga fungu la ujenzi. Ili kuhakikisha usalama barabarani na kuchochea ufanyaji biashara hasa nyakati za usiku, serikali imepanga kutumia TZS bilioni 1.3 kuweka taa za barabarani katika maeneo ya Mangaka, Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara.
Mbali na miradi hiyo, akiwa ziarani mkoani humo amezindua na kukagua miradi ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini Mtwara ambayo itatoa ahueni kubwa kwa wananchi ambao awali walifuata matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi mkoani Dar es Salaam.