Serikali imetangaza kuwa huduma za vipimo vya awali kwa wajawazito ambazo zinahusisha kupima wingi wa damu, mkojo ili kuangalia wingi wa protini, shinikizo la damu pamoja na kusikiliza mapigo ya moyo ya mtoto, zitatolewa bure.
Kutolewa bure kwa vipimo hivyo muhimu kutawawezesha wajawazito kujua mwenendo wa ujauzito, kuepuka kifafa cha mimba na vifo vya mama na mtoto ambapo lengo la Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) ni kupunguza vifo vya uzazi kutoka vifo 321 kwa vizazi 100,000, hadi vifo 220 na vifo vya watoto kutoka vifo 51 kwa vizazi hai 1,000 hadi vifo 40.
Aidha, hatua hii itaongeza zaidi idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki pamoja na kujifungulia kwenye vituo vya afya ambapo Serikali imeahidi itahakikisha upatikanaji wa 100% wa dawa za kuzuia kutoka damu wakati wa kujifungua, dawa za kuongeza damu na dawa za kuzuia kifafa cha mimba katika vituo vyote afya vya umma.
Hatua hizi ni mwendelezo wa kazi kubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu wa kujenga vituo vya afya, kuboresha miundombinu ya afya nchi nzima, kuajiri maelfu ya watumishi wa afya pamoja na kununua vifaa tiba, hivyo kuiarisha huduma za afya vijijini ambapo awali hali ilikuwa ngumu zaidi.
Imani juu ya huduma za afya zinazoendelea kutolewa kwenye vituo vya afya imeendelea kuongezeka kwani kwa mujibu wa Utafiti wa Demografia na Afya mwaka 2022, idadi ya wajawazito waliotembelea kliniki walau mara nne kati ya wajawazito 100 imeongezeka kutoka 53 mwaka 2015/16 hadi 65 mwaka 201/22 kati huku wanaojifungua chini ya uangalizi wa mtoa huduma mwenye ujuzi ikiongezeka kutoka 66 hadi 85 katika kipindi hicho.