Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limetoa takwimu zinazoonesha kuongezeka kwa pato la Taifa la Tanzania kutoka Dola za Marekani Bilioni 69.9 (TZS trilioni 163.5 trilioni) kwa mwaka 2021, wakati ambapo Rais Samia alipoingia madarakani hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 85.42 (TZS trilioni 200) kwa mwaka huu wa 2023,
Huu ni ukuaji mkubwa zaidi katika kipindi cha muda mfupi cha uongozi wa awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ndani ya miaka miwili pato hilo limeongezeka kwa Dola za Marekani Bilioni 16 (TZS trilioni 37.616) ikilinganishwa na ukuaji wa miaka sita ya awamu ya tano ambapo pato hilo lilikua kwa Dola za Marekani Bilioni 12 pekee (TZS trilioni 28.212).
Vilevile IMF imeonesha kuwa kwa mwenendo uliopo hadi mwaka 2028 Tanzania kutakuwa na watu milioni 73.36 huku pato la Taifa likitarajiwa kukua hadi dola bilioni 136.09 (TZS trilioni 318.8) na pato la mtu mmoja mmoja likitarajiwa kukua hadi dola 1,860 (TZS milioni 4.3), huku kasi ya ukuaji wa uchumi ikitarajiwa kuwa asilimia 7.
Ukuaji huu wa uchumi ni matokeo ya jitihada za makusudi za Mheshimiwa Rais ambapo tangu alipoingia madarakani Machi mwaka 2021, ametekeleza sera rafiki kwa sekta binafsi, ambayo imeongeza kasi ya uwekezaji, biashara na ukuaji wa uchumi nchini huku akifungua fursa za ajira kwa wananchi kote nchini.
Kazi hii kubwa ya ukuaji wa uchumi ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inaeleza lengo la kukuza kwa Pato la Taifa pamoja na kujenga uchumi wa kisasa, shirikishi na shindani, utakaowezesha ustawi wa wananchi.