Waswahili wana msemo wao usemao “Lisilo budi hutendwa”, kwa kadhia ya upatikanaji
wa maji waliyoipata wakaazi wa mkoa wa Dar es Salaam na mkoa wa Pwani mtawalia
ndani wiki kadhaa nyuma, serikali ya Rais Samia Suluhu haikuwa na budi kuidhinisha
utekelezaji wa ujenzi wa bwawa la Kidunda.
Leo tarehe 11.11.2022 Rais Samia Suluhu ameshuhudia utiaji wa saini wa ujenzi wa mradi
wa bwawa kubwa la Kidunda, ambapo saini hiyo ilifuatia na kumkabidhi mkandarasi eneo
la mradi tayari kwa kuanza utekelezaji.
Wazo la kujenga bwana la Kidunda lilikuwepo tangu baada ya nchi yetu kupata Uhuru
mwaka 1961. 1961 chini ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) Tanzania ilifanya upembuzi
yakinifu ya ujenzi wa bwawa hilo, 1992 ukafanyika utafiti kwa mara ya pili, utafiti wa tatu
ukafanywa Shirika la Maendeleo ya Japan (JICA) mwaka 1994 na 2008 Wizara ya Maji na
Umwagiliaji ikafanya nayo upembuzi yakinifu ya ujenzi wa mradi huo mkubwa.
Katika nyakati zote hizo, licha ya maazimio mengi kuwekwa bungeni, mradi huo ulikuwa
ni kitendawili kigumu kwenye utekelezaji kutokana na ufinyu wa bajeti.
Baada ya miaka zaidi ya sitini leo tarehe 11.11.2022 Rais Samia Suluhu anashuhudia utiaji
wa saini wa mradi mkubwa wa ujenzi wa bwana la Kidunda. Mradi huu unakwenda kuwa
suluhu ya kudumu ya upungufu wa maji katika jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani na
habari njema zaidi utatekelezwa kwa fedha za ndani.
Bwawa la Kidunda litakuwa na uwezo wa kukusanya na kuhifadhi maji mita za ujazo
milioni 150, na kisha kutiririsha maji hayo kwenye Mto Ruvu nyakati za uhaba na
kupelekea uhakika wa kupatikana maji katika jiji la Dar es Salaam na Pwani ambao
hutegemea maji katika Mto Ruvu kwa zaidi ya asilimia 90.
Mradi huu utatumia gharama ya shilingi bilioni 329 na utatumia muda wa miaka miwili
na miezi sita kukamilika. Mradi huu wa bwawa la Kidunda ni suluhu ya kudumu ya
kadhia ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani