Rais Samia anavyoacha alama za kipekee katika soka la bongo

Zaidi ya mashabiki 60,000 walioujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam walilipuka kwa shangwe baada ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo dhidi ya Guinea na kuibuka na ushindi wa goli 1-0, ushindi uliomaanisha kuwa Tanzania kwa mara ya nne imefuzu kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 itakayofanyika nchini Morroco

Tanzania inafuzu kushiriki michuano hii kwa mara ya nne ikiwa imefanya hivyo mwaka 1981, 2019, 2023 na sasa 2025.

Kwa hatua hii Mheshimiwa Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia katika vitabu vya kumbukumbu na historia ya michezo nchini kwa kuwa Rais ambaye chini ya uongozi wake timu ya Taifa imefanikiwa kufuzu kushiriki mashindano haya makubwa zaidi kwa ngazi ya nchi barani Afrika mara mbili tena mfululizo.

Mafanikio haya hayatokei kwa bahati mbaya na ni dhahiri kuwa ni matokeo uongozi thabiti na motisha kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Sote tunafahamu namna ambavyo amekuwa akichochea timu za Taifa na hata vilabu vinavyoshiriki michuano ya kimataifa kupata matokeo chanya kwa kuweka motisha ya goli la Mama.

Katika mchezo dhidi ya Ethiopia uliofanyika nchini Congo, Rais Samia alitoa ndege maalum iliyowapeleka wachezaji katika mchezo ule na kuwawezeshea kurejea kwa wakati nchini kujiandaa na mchezo dhidi ya Guinea ambao ndio umeipatia Tanzania tiketi ya kufuzu Afcon 2025.

Ushindi dhidi ya Guinea ulichagizwa kwa kiasi kikubwa na nguvu ya mashabiki zaidi ya 60,000 walioujaza uwanja wa Taifa. Nakukumbusha tu mashabiki hawa wote waliingia bure kwani Rais Samia aliwalipia wote viingilio ili tu wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono Taifa Stars.

Habari njema zaidi ni kwamba baada ya Afcon 2025, michuano inayofuata mwaka 2027 Tanzania pia imo ndani kwani kwa mara ya kwanza michuano hii itafanyika katika ardhi ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda hivyo tayari tuna tiketi ya moja kwa moja. Mashindano haya kuja Afrika Mashariki yanatokana na utayari na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa mataifa haya akiwemo Rais Samia.

Michezo ni ajira, michezo ni furaha michezo inaunganisha Taifa na hakika chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania ina furaha na iko tayari kuiunga mkono Taifa Stars ikiwa inapeperusha bandera ya Taifa katika viunga vya Morocco mwaka 2025