Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameanza ziara yake rasmi nchini Uturuki kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Recep Erdoğan. Ziara hiyo ya kimkakati inatarajiwa kuwa na matokeo chanya kidiplomasia, kiuchumi na kimaendeleo ambapo inafanyika kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 14 (tangu mwaka 2010), na miaka saba tangu ziara ya Rais Erdoğan nchini.
Tanzania na Uturuki zina uhusiano wa miaka 61 (tangu mwaka 1963), ambapo Uturuki ilifungua ubalozi wake nchini mwaka 1969, ikaufunga mwaka 1984 na kuufungua tena mwaka 2009, na hivyo kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na uhusiano baina ya mataifa haya.
Malengo makuu matatu ya ziara hiyo ya kimkakati ni kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo, kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, na kuendeleza ushirikiano wa kimaendeleo. Maeneo hayo yanatarajia yatapewa uzito katika mazungumzo atakayofanya na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Erdoğan.
Nchi hizi zina ushirikiano mkubwa kwenye biashara na uwekezaji ambapo Uturuki ni miongoni mwa nchi 20 zenye uchumi mkubwa zaidi duniani imewekeza nchini zaidi ya TZS trilioni 1.3 na kuzalisha ajira zaidi ya 6,700. Kwa upande wa Tanzania, huuza wastani wa bidhaa zenye thamani ya TZS bilioni 41 kila mwaka nchini Uturuki.
Mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaotekelezwa na kampuni ya Uturuki, Yapi Merkez ni kielelezo kikubwa cha ushirikiano baina ya nchi, na ziara hii inatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza kasi ya kutekeleza mradi huo utakaobadili maisha na uchumi wa Tanzania. Aidha, Uturuki ni mshirika mkubwa katika kukuza utalii nchini ambapo safari za ndege za moja kwa moja kwenda Dar es Salaam na Kilimanjaro zimerahisisha usafiri wa watalii, sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wetu.
Katika kufanikisha lengo la kufungua fursa mpya za ushirikiano, akiwa nchini Uturuki, Mheshimiwa Rais Samia atashiriki jukwaa la uwekezaji pamoja na kuzungumza na kampuni 15 kubwa zaidi nchini humo na kuwashawishi kuja kuwekeza nchini. Mheshimiwa Rais katika ziara hiyo ameambatana pia na wafanyabiashara kutoka Tanzania, ikiwa ni mkakati wake wa kufungua fursa za ubia, na kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania.
Kama sehemu ya awali ya matunda ya ziara hiyo, Tanzania na Uturuki zitasaini hati nane za makubalino ya ushirikiano ambazo zitaongezea kwenye maeneo ya sasa ya ushirikiano ikiwemo usafiri wa anga, afya, maji na elimu.
Katika hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Ankara ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Utururki kinatarajiwa kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Heshima ya Udaktari katika Uchumi ikiwa ni njia ya kutambua mchango wa uongozi wake katika kuimarisha mageuzi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Mbali na hayo machache kati ya mengi, ziara hiyo ni heshima kubwa kwa Mheshimiwa Rais Samia na kwa Tanzania kama nchi, na inajenga taswira chanya ya namna Uturuki inaichukulia Tanzania kama mshirika wake kwani ziara za kitaifa zinahitaji maandalizi makubwa kwa nchi mwenyeji, hivyo hazifanywi kwa kila kiongozi, ikilinganishwa na ziara za kikazi au ziara binafsi.