Miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa yaliyoboresha sekta ya afya nchini na kufanya huduma za afya kuwa karibu, bora na nafuu zaidi.
Vituo vya kutolewa huduma za afya (zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa, rufaa na za kanda) 1,061 vimejengwa ambapo ni wastani wa vituo 353 kila mwaka. Ujenzi wa vituo hivi umeenda sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa ambavyo vimetoa ahueni kubwa kwa wananchi.
MAMA amenunua mashine mpya za CT Scan 27, na kufanya mashine hizo nchini kufikia 45, kutoka 13 za awali. Hivi sasa mashine hizo za kiuchunguzi zinapatikana kwenye hospitali zote za rufaa za mikoa. Manufaa makubwa yanaonekana ambapo awali wakazi wa Katavi walilazimika kusafiri zaidi ya kilomita 600 kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Mbeya, lakini sasa huduma hiyo inapatikana mkoani mwao.
Tangu tupate uhuru, kwa miaka 61, Tanzania ilinunua mashine za MRI saba, lakini ndani ya miaka mitatu MAMA amenunua mashine sita na kuifanya nchi kuwa na MRI 13 ambazo zimefungwa kwenye hospitali za rufaa za kanda.
Mashine za X-Ray ambazo awali hazikupatikana kwa wingi kwenye vituo vya afya, sasa zimejaa tele baada ya kununuliwa kwa Digital X-Ray 199, na kuifanya nchi kuwa namashine 346. MAMA pia amenunua mashine za ultrasound 192 na kuifanya nchi kuwa na mashine 668 ambazo ni muhimu hasa katika kufuatilia ukuaji wa mimba.
Vifaa tiba vingine vilivyoongezwa ni Echocardiogram kutoka 95 mwaka 2021 hadi 102 mwaka 2024, Cathlab kutoka moja mwaka 2021 hadi nne mwaka 2024 pamoja na PET Scan ambayo ndiyo ya kwanza nchini mwetu. Vitanda vipya 40,078 vya kulaza wagonjwa, vitanda vipya 1,104 vya vya ICU pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa kufikia asilimia 84 kutoka asilimia 58 mwaka 2022.
Mageuzi haya yaliyofanyika yamewezesha kupungua kwa vifo vinavyoepukika ikiwemo vifo vya wajazito na watoto chini ya miaka mitano, kumeimarisha huduma za ubingwa na ubingwa bobezi na hivyo kufanikisha azma ya utalii wa kimatibabu pamoja na kupunguzia wananchi gharama kwa huduma ambazo walikuwa wanazifuata nje ya nchi.
MAMA anaendeleza mageuzi haya akiamini kwamba kufanikiwa kwa mipango mingine yote kunategemea hali ya afya ya wananchi ambao ndio nguvu kazi na injini ya mabadiliko.