BoT kununua dhahabu inathibitisha nia ya Serikali kuimarisha utulivu wa kiuchumi

Dar es Salaam, Tanzania – Serikali chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uchumi wa nchi, ambapo sasa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua kubwa ya kimkakati ya kununua dhahabu ya ndani ili kuimarisha hifadhi ya fedha za kigeni na kuongeza nguvu ya shilingi ya Tanzania.

Tayari BoT inanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa ndani kwa kutumia shilingi ya Tanzania ambapo tayari imenunua kilogramu 418, lengo likiwa ni kununua kilogramu 6,000 katika mwaka wa fedha 2023/24.

Hatua hii muhimu ina manufaa mbalimbali kwa taifa na wananchi kwa kununua dhahabu kwa ajili ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni, taifa letu linajikinga dhidi ya athari zitokanazo na mabadiliko ya ghafla (kutokuwepo kwa uhakika) ya kiuchumi wa kimataifa. Dhahabu imekuwa kimbilio la thamani kwa miongo mingi wakati wa migogoro ya kiuchumi na kisiasa duniani. Kwa hivyo, kwa kuchanganya dhahabu katika akiba ya fedha za kigeni, Tanzania inaweza kusaidia kulinda thamani ya shilingi ya nchi wakati wa mazingira magumu ya kiuchumi duniani.

Pia, hatua ya kununua dhahabu kutoka kwa wazalishaji wa ndani kutachangia kukuza uchumi wa ndani kwani itachochea uzalishaji wa dhahabu. Kukua kwa uzalishaji kunaenda moja kwa moja na kuongezeka kwa ajira, kwani shughuli za uchimbaji na biashara ya dhahabu zinahitaji wafanyakazi, na pia ongezeko la wachimbaji litanufaisha sekta nyingine zinazofungamana na sekta hiyo ikiwemo ya huduma (chakula, maji, nishati, mawasiliano).

Uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania wa kununua dhahabu kwa ajili ya kuongeza akiba ya fedha za kigeni na kulinda uchumi unathibitisha nia ya serikali ya kusimamia utulivu wa kiuchumi na kujenga nguvu za kifedha, hatua ambayo inaweza kuwa na athari chanya kwa maendeleo na ustawi wa nchi.