Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema anatambua umuhimu wa katiba mpya kama ambavyo maoni ya makundi mbalimbali, ikiwemo kikosi kazi, yaliyotolewa na kusisitiza kuendelezwa kwa mchakato huo ambao ulikwama tangu mwaka 2014.
Licha wa umuhimu huo ametahadhari kuwa upatikanaji wa katiba mpya ni mchakato na kwamba mchakato huo sio mali ya wanasiasa bali ni ya Watanzania wote, hivyo amewataka wanasiasa kutokuhodhi sauti kwenye mchakato huu.
“Katiba ni ya Watanzania, awe ana chama, awe hana, awe ana dini, awe hana, awe mrefu, awe mfupi, mnene, mwembamba, mkubwa, mdogo. Kwa hiyo matengenezo yake yanahitaji tafakuri kubwa sana,” amesema Mheshimiwa Rais.
Hata hivyo, amesema kuwa katiba si kitabu, bali ni misingi ya maadili, itikadi na namna ambavyo Watanzania wanakubaliana kuendesha Taifa lao, hivyo, makubaliano hayo yanaandikwa, hivyo, haiwezi kuwa sawa na nchi nyingine.
“Tunaanza na elimu Watanzania wajue [katiba] ni kitu gani […] Kwa hiyo tusiwaburuze wananchi. Katiba viongozi wa kisiasa si mali yetu, ni mali ya Watanzania. Tunachokitaka kwenu ni maoni katiba iweje,” ameongeza.
Aidha, ameongeza demokrasia lazima iakisi namna watu ndani ya nchi yanavyoendesha masuala yao ikiwemo tamaduni, maadili, mila, desturi, na kwamba huwezi kuchukua demokrasia kutoka nchi nyingine na kuiingiza nchini bila kuzingatia masuala ya ndani.