Mheshimiwa Rais abadili miundo ya wizara ili kuchochea ufanisi na maendeleo

Kufuatia kutungwa kwa Sheria ya Mipango ya Taifa ya Mwaka 2023 pamoja na uamuzi wa kuhamishia masuala ya uwekezaji Ofisi ya Rais, hivyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko madogo ya miundo ya wizara na kufanya uteuzi wa viongozi.

Mheshimiwa Rais ameunda Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ambapo amemteua Prof. Kitila Mkumbo kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. Prof. Mkumbo ni mbunge wa jimbo la Ubungo.

Pili, ameunda Wizara ya Fedha ambapo amemteua Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Fedha. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Nchemba alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Pia, ameunda Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo amemteua Dkt. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa wizara hiyo. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Kijaji alikuwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Amemteua Lawrence Mafuru kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa. Kabla ya uteuzi huu Mafuru alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango (Usimamizi wa Uchumi).

Mwisho, amemteua Elijah Mwandumbya kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha (Usimamizi wa Uchumi). Kabla ya uteuzi huo Mwandumbya alikuwa Kamishna, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha na Mipango.