Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa na mchango muhimu katika ukuaji wa uchumi, ajira, mapato ya serikali na ukuzaji wa sekta nyingine. Uwezo wake wa kuhudumia mizigo umeendelea kuimarika ambapo makasha yaliyohudumiwa yameongezeka kufikia makasha 63,529 mwaka 2022 kutoka makasha 56,198 mwaka 2021.
Ripoti ya Benki ya Dunia (The Container Port Performance Index 2022) imeiweka Bandari ya Dar es Salaam katika nafasi ya kwanza kwa ufanisi Afrika Mashariki ikiipita Bandari ya Mombasa nchini Kenya kutoka na kuimarika kwa ufanisi ambao umepunguza kwa muda ambao meli zinatumia bandarini, jambo ambalo ni muhimu kwa kukuza ushindani wa kibiashara.
Katika ripoti hiyo ya dunia imeiweka Bandari ya Dar es Salaam katika nafasi ya 312, huku Mombasa ikiwa nafasi ya 326. Dar es Salaam imepanda kwa nafasi 49 ikitoka nafasi ya 361 mwaka 2021, huku Mombasa ikishuka kwa nafasi 30 kutoka 296 mwaka 2021.
Mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji wa takribani bilioni 1 uliofanyika bandarini ukihusisha upanuzi wa gati namba 1 hadi 7 kwa kuongeza kina kutoka mita 7 hadi mita 14.7 ambazo zinaruhusu meli kubwa yenye uwezo wa kubeba mizigo tani 6,500 kutia nanga.
Maboresho mengine ni mashine za kisasa za kupakua mizigo ambazo zinafanyakazi kwa kasi mara mbili ya awali mikakati ambayo sambamba na uimiarisha matumizi ya TEHAMA imeongeza mara mbili idadi ya meli za mizigo zilizokuwa zikihudumiwa bandarini.
Aidha, ikilinganishwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), bandari ya Dar es Salaam imepanda kwa nafasi tatu kutoka nafasi ya 9 mwaka 2021 hadi nafasi ya 6 mwaka 2022. Ukuaji huu umeendelea kuwa na matokeo chanya katika kuvutia uwekezaji na biashara, ajira zaidi na kuongeza mapato ya Serikali yanayorudi kuwahudumia Watanzania.