Tanzania ya pili Afrika matumizi ya TEHAMA kuhudumia wananchi

Tanzania imetajwa na Benki ya Dunia (WB) kuwa nchi ya 26 duniani na ya pili barani Afrika kwa kuwa na mfumo madhubuti wa matumizi ya Teknolojia ya Mawasiliano na Habari (TEHAMA) katika kutoa huduma kwa wananchi, utaratibu ambao unawezesha huduma kupatikana kwa wakati na unafuu.

Katika utafiti huo wa GovTech Maturity Index (GTMI) 2022 uliofanywa na Benki ya Dunia na kuhusisha nchi 198 umeiweka Tanzania katika Kundi A ikipanda kutoka Kundi B mwaka 2021 ambapo kwa dunia ilikuwa nafasi ya 90 na Afrika nafasi ya tano, ambapo matumizi ya TEHAMA yamekuwa kwa asilimia 0.86 kwa mwaka uliopita.

Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwenye kutoa huduma kwa umma, ambapo hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alishuhudia utiaji saini mikataba ambayo itakwenda kufikisha huduma ya mawasiliano kwa Watanzania zaidi ya milioni 8, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

Utafiti huo umeonesha kuwa sekta za elimu, afya, huduma za fedha kwa simu na kilimo ndizo sekta zinazoongoza kutoa huduma kwa umma kwa kutumia TEHAMA. Mkakati huo umeendelea kufanikiwa kutokana na hatua za Serikali kuweka mazingira rafiki na kuwainua wabunifu wa kidijitali.

Kufikishwa kwa mawasiliano kwenye vijiji ambavyo havikuwa na huduma hiyo hapo awali kutapanua zaidi wigo wa Watanzania wanaoweza kunufaika na huduma za kidijitali za Serikali, na hivyo kukuza kiwango cha Tanzania kwa upande wa Afrika na dunia katika tafiti zijazo.