Utayari wa kisiasa wa Rais Samia utakavyoipa Tanzania katiba bora

Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kufufua mchakato wa kuipata Katiba Mpya uliokwama tangu mwaka 2014 umeonesha utayari wa kisiasa wa ofisi hiyo ya juu zaidi nchini kuleta Mabadiliko (Reformation) kama alivyoeleza kwenye msingi wa 4R za uongozi wake.

Aidha, kurejeshwa mezani kwa mchakato huo kumethibitisha pamoja na mambo mengine kuwa Rais Samia ni msikivu, na anafanyia kazi maoni anayopokea kwa pendekezo la kufufua mchakato huo lilitolewa na kikosi kazi alichokiunda mwaka jana kwa ajili ya kutathmini hali ya kisiasa nchini.

Kama wasemavyo Wahenga kuwa Ukimulika Nyoka Anzia Miguuni Pako, ndivyo Rais alivyofanya kwani Kamati Kuu ya CCM, chama anachokiuongoza, Juni 2022 iliielekeza Serikali kuangalia namna ya kufufua mchakato huo ambapo sasa TZS bilioni 9 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.

Utayari wake wa kisiasa umeweza kuufikisha mchakato hadi ulipo sasa ambapo mwanga unaonekana kuelekea kulifikia lengo, huku wadau mbalimbali wakimpongeza kwa kuvuka vikwazo vyote ndani ya Serikali na chama chake kwani amewahi kusema yeye mwenyewe kuwa uamuzi huo si kila mmoja anakubaliana nao.

Amepongezwa pia kwa namna anavyoufanya mchakato huo kuwa shirikishi ukihusisha majadiliano ya vyama vyote, wanadau na wananchi kwa ujumla akiamkini kuwa maboresho yanayokwenda kufanyika ni kwa ajili ya manufaa ya Watanzania, hivyo ni lazima washirikishwe.