Wakazi 644 wa Magomeni Kota mkoani Dar es Salaam waligoma kusaini mkataba wa kuanza kununua nyumba za eneo hilo kwa madai kwamba bei pamoja na muda wa malipo uliopangwa haukuwa rafiki kwao na wala hauendani na hali zao za kiuchumi ambapo walipaza sauti zao kumuomba Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo.
Mwenyekiti wa Wakazi hao wa Magomeni Kota, George Abel alisema bei za nyumba hizo ni kubwa, zisizoendana na uwezo wao, hivyo hawawezi kuimudu licha ya Serikali kuzishusha bei ikilinganishwa na hali ya soko.
Wakazi hao walipaza sauti wakimuomba Rais Samia kuongezewa muda wa kulipia nyumba hizo kutoka miaka 15 iliyokuwepo awali hadi miaka 30 hali ambayo itapunguza kwa asilimia 100 kiasi ambacho wananchi hao wanapaswa kulipa kila mwezi.
Rais Samia Suluhu Hassan, aliye msikivu na anayejali wananchi wote, alipokea maombi hayo na ameyafanyia kazi na sasa wananchi wa Magomeni Kota watalipa nyumba zao kwa kipindi cha miaka 30 kama walivyoomba, muda ambao wakazi wote wa eneo hilo wamekiri kuwa ni rafiki na kila mmoja amekiri ataweza kukamilisha malipo yaliyopunguzwa
Ikumbukwe pia Machi 23, 2021, wakati Rais Samia akizindua nyumba hizo aliitaka TBA kupunguza gharama za uuzaji wa nyumba hizo kwani zipo juu kwa wananchi wa kawaida, hivyo pamoja na kupunguzwa bei pia sasa wananchi watalipa nyumba hizo kwa muda mrefu zaidi
“Pamoja na kuwa kipato chetu kimekuwa kidogo kwa sababu ya kustaafu lakini, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kupata unafuu wa nyongeza hii ya muda, kwa sasa naamini sote tunaweza kujitahidi kukamilisha jambo hili (malipo),” alisema Ramadhan Mkenze mkazi wa Magomeni Kota.