Miaka miwili ya Mama: Uwekezaji wa trilioni 17 wazalisha maelfu ya ajira

Katika kipindi cha mwaka 2021 hadi Januari 2023 Serikali imesajili miradi ya uwekezaji 537 yenye thamani ya TZS trilioni 17, ikiwa ni matokeo mazuri katika mkakati wa Mheshimiwa Rais wa kukuza biashara na uwekezaji nchini.

Ongezeko la usajili wa miradi hiyo linatarajiwa kutoa ajira takribani 92,770 ikiwa ni kiwango kikubwa zaidi kuwahi kuandikishwa katika kipindi chochote tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.

Hatua alizochukua Rais Samia kuboresha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuimarisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja na maboresho ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania zimevutia wawekezaji wapya, zimetatua changamoto zilizokuwa zikiwakabilia wafanyabiashara na kuvutia wawekezaji na kurahisisha utoaji huduma.

Aidha, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Mauzo ya Nje (EPZA) imesajili miradi 38 yenye thamani ya TZS bilioni 327.7 na mauzo nje yenye thamani ya TZS bilioni 448.2.

Miradi hiyo ni mahsusi katika sekta zinazozalisha bidhaa zitokanazo na kilimo, bidhaa za viwandani, bidhaa za mifugo, bidhaa za kemikali, bidhaa za madini na bidhaa za misitu.

Kuendelea kuongezeka kwa uwekezaji nchini kunakuza mzunguko wa fedha nchini, kunajenga imani ya wawekezaji waliopo pamoja na kuvutia uwekezaji zaidi.