Rais Samia afungua fursa: Mchango wa Diaspora wavuka trilioni 2

Moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoiweka wazi baada ya kuingia madarakani ni kutoa fursa zaidi kwa Watanzania waishio nje kushiriki katika shughuli za maendeo na kijamii nchini kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha kufanya shughuli zao nchini.

Mafanikio yameendelea kuonekana ambapo kwa mwaka 2022 pekee diaspora walituma nchini TZS trilioni 2.6, na pia wamewekeza kupitia ununuzi wa nyumba na viwanja wenye thamani ya TZS bilioni 4.4 na ununuzi wa hisa za TZS bilioni 2.5.

Ili kupanua ushiriki wa diaspora katika maendeo ya Tanzania Serikali inatarajia kuwa imekamilisha mfumo wa kidigitali wa uandikishaji wa diaspora Juni mwaka huu ili kuwezesha ukusanyaji endelevu wa takwimu zao.

Mbali na kutuma fedha na kuwekeza nchini, diaspora pia huchangia ukuaji wa uchumi kwa kutangaza fursa za kiuchumi, biashara, utalii na uwekezaji zinazopatikana nchini. Mchango mwingine ni kuleta mitaji, utaalam na teknolojia ambavyo huchangia katika kukuza uzalishaji wa mazao, bidhaa na huduma mbalimbali zenye tija kiuchumi.

Hadi sasa idadi ya diaspora wa Tanzania ni milioni 1.5, idadi ambayo Rais anaamini itakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi ikiwekewa mazingira rafiki.