Benki ya Dunia imeimwagia sifa Tanzania chini Rais Rais Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruk amesema Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha ambapo licha ya changamoto za UVIKO-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathimini ya benki hiyo inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.
“Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa usimamizi mahiri wa masuala ya uchumi mpana, si tu kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana” amesema Dkt. Ngaruko
Aidha, amepongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa benki yake itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi.
Mpaka sasa Benki ya Dunia imewekeza zaidi ya TZS trilioni 16.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya 29 nchini ambapo kati ya miradi hiyo, 24 yenye thamani ya TZS trilioni 15 ni ya kitaifa, na mingine 5 yenye thamani ya TZS trilioni 1.7 ni ya kikanda.