Dodoma, London, Maputo: Septemba ya Rais Samia na Diplomasia ya Uchumi

Septemba 17 mwaka huu Rais Samia aliondoka nchini kuelekea Uingereza kuhudhuria mazishi wa Malkia Elizabeth II baada ya kualikwa kama mmoja wa viongozi wa nchi wananchama wa Jumuiya ya Madola. Watu mashuhuri dunianiani takribani 500 walipewa mualiko huo ambao ulizingatia si tu uanachama wa Jumuiya ya Madola lakini pia rekodi ya haki za binadamu kwa kiongozi mwalikwa na nchi anayotoka.

Pamoja na mambo na kupata nafasi ya kukutana na viongozi wa mataifa mengine, kuhudhuria mazishi hayo kitendo hicho ni ishara ya uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza pamoja na jumuiya hiyo ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Tanzania kwa kwa zaidi ya miaka 50 hivi sasa. Kwa mujibu wa takwimu za kituo cha uwekezaji Tanzania, Uingereza ni moja ya wawekezaji wakubwa zaidi Tanzania ikiwa na zaidi ya 30% ya uwekezaji wa Tanzania unaotoka nje (FDI). Mfano kati ya mwaka 1990 hadi 2013 Uingereza iliwekeza Tanzania zaidi ya shilingi Trilioni 8.5 ikizalisha ajira 271,000 kwa Watanzania.

Baada ya shughuli hiyo, Rais Samia alielekea nchini Msumbiji kwa  ziara ya kiserikali ya siku tatu ambayo imekuwa na manufaa makubwa kati ya mataifa haya jirani katika kuimarisha ushirikiano wake. Tanzania na Msumbiji zina uhusiano mkubwa wa kihistoria. Nchi hizi zinashea mpaka wa pamoja wa zaidi ya kilometa 800, eneo muhimu katika usalama na uchumi hasa nyakati hizi za ugunduzi wa gesi kwenye mikoa ya kusini mwa nchi yetu.  Mwenendo huu unafanya Msumbiji kuwa mbia muhimu wa Tanzania katika uchumi, ulinzi na usalama.

Ili kuimarisha ulinzi na usalama ambao ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi, Tanzania na Msumbiji zilitia saini hati mbili za makubaliano, moja ikiwa ni ushirikiano katika masuala ya ulinzi na ya pili ikiwa Uratibu wa Huduma za Utafutaji na Uokoaji ikikumbukwa kuwa Taifa hilo limekuwa likipambana na magaidi katika jimbo la Cabo Delgado ambalo kwa Tanzania limepakana na mkoa wa Mtwara.

Rais Samia alisema amani iliyopo kati ya nchi hizi, inatokana na vyama vilivyopo madarakani akimaanisha CCM kwa upande wa Tanzania na FRELIMO kwa upande wa Msumbiji, hivyo aliomba tunu hiyo ilindwe.

Rais Samia Suluhu amewataka Watanzania wanaoishi na kufanya biashara nchini Msumbiji kutumia fursa ya ushirikiano wa hizo mbili kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

“Tunajua kwamba kuna Watanzania wengi wanaoishi na kufanya biashara Maputo, nikiwa na kaka yangu Nyusi tulikubaliana kuwaeleza watu wetu kushirikiana kufanya biashara na kuwekeza kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema Rais Samia.

Katika elimu, Tanzania imeonesha utayari wa kutengeneza mpango mkakati wa kupeleka walimu nchini Msumbiji kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili hasa kwa shule za msingi. Hii ni fursa kwa Tanzania kukuza utamaduni wake na ajira kwa watu wake.

Rais Samia alihimiza matumizi ya Kiswahili kwa kuwa kuna baadhi ya nchi baada ya kupata uhuru hazikufanya juhudi za kutosha kutumia lugha hiyo na kuendelea kutumia za kigeni.

Aidha, nchi zote mbili zimehuisha mfumo wa kubadilishana wanafunzi ujulikanao kama (TAMOSE) ulioisha muda wake mwaka 2015 kwa kunufaisha wanafunzi 369, na kukubaliana kuongeza muda tena.

Comments

  • ZAP

    March 21, 2024 at 8:07 am
    Reply

    Zaproxy dolore alias impedit expedita quisquam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *