Wachina Kariakoo
-
Kwa mara nyingine Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha namna anavyosikiliza na kuzipatika majawabu changamoto za wananchi wake, ambapo sasa Serikali imeweka zuio katika baadhi ya biashara kutofanywa na raia wa kigeni. Uamuzi huo umetokana na malalamiko ya wananchi juu ya uwepo wa raia wa kigeni kufanya kazi ambazo zingeweza kufanywa na wazawa. Kwa mujibu wa Amri ya Leseni za Biashara (Zuio la Shughuli za Kibiashara kwa wasio Raia), 2025, serikali imezuia wageni kufanya aina 15 za biashara, zikiwemo biashara ya bidhaa ya jumla na rejareja, isipokuwa supermarkets au maduka yanayouza kwa jumla kwajili ya wazawa. Biashara nyingine zilizozuiwa ni huduma ya uwakala wa fedha kwa simu, ufundi wa simu na bidhaa za kieleketroniki, uchimbaji mdogo, kuongoza watalii, huduma za posta na usafirishaji vipeto, uanzisha na uendeshaji wa redio na televisheni, uendeshaji wa maeneo ya makumbusho pamoja na udalali. Aidha, wamezuiwa kufanya biashara ya huduma za forodha na usafirishaji, ununuzi wa mazao shambani, umiliki na uendeshaji wa mashine za kamari isipokuwa ndani ya viunga vya casino pamoja na umiliki na uendeshaji wa viwanda vya chini na vidogo. Kumekuwa na malalamiko ya wananchi kuwa raia wa kigeni, hasa wa China wanafanya biashara za wazawa ikiwemo uuzaji wa nguo Kariakoo, udalali wa nyumba pamoja na uwakala wa fedha. Hatua hii ni mwendelezo wa Mheshimiwa Rais kukabiliana na changamoto ya ajira nchini, hasa kwa vijana, ambapo pia serikali yake imeendelea kutoa mikopo, kupanua fursa za elimu ya ufundi stadi, kuwapatia elimu ya kilimo-biashara pamoja na kufungua fursa za masoko ndani na nje ya nchi. Uamuzi huu umepongezwa na wananchi, hasa kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wengi wamempongeza Mheshimiwa Rais kuwa amesikia na kujibu kilio chao cha muda mrefu. Read More