Uwekezaji Tanzania (TIC)
-
Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeonesha kuwa thamani ya miradi ya uwekezaji imeongezeka kwa mwezi mmoja kufikia TZS trilioni 2.33 kwa Agosti mwaka huu kutoka TZS trilioni 1.06 kwa Julai mwaka huu, sawa na ukuaji wa asilimia 120. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kuwa miradi ya uwekezaji imeongezeka kufikia 58 kutoka 40 katika kipindi tajwa, ambapo kwa miradi iliyosajiliwa Agosti mwaka huu inatarajiwa kuzalisha ajira 25,700. Ongezeko la miradi limeendelea kusadifu mikakati na mkazo uliowekwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kilimo ili kuboresha maisha ya Watanzania ikizangatiwa sekta hii kwa takwimu za mwaka 2021 ilichangia asilimia 26.1 katika Pato la Taifa, ilitoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda. Matokeo ya kazi kubwa anayofanya Mheshimiwa Rais imeendelea kuonekana ambapo thamani ya uwekezaji kwenye kilimo imeongezeka kwa zaidi ya TZS bilioni 275.53 kufikia TZS bilioni 849.13 kutoka TZS bilioni 571.1 kwa Julai mwaka huu. Wakati uwekezaji kwenye kilimo ukiendele kukua, Serikali imeendelea kuchua hatua kumwezesha mkulima mdogo ikiwemo kuimarisha huduma za ugani, kutoa ruzuku na pembejeo za kilimo, kufungua fursa za masoko, kujenga mifumo ya umwagiliaji, kutoa elimu ya kilimo cha kisasa, hasa kwa vijana, pamoja na afua nyingine ili kuwezesha kilimo kuchangia asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo mwaka 2030. Wanazuoni wamepongeza mageuzi yanayoendelea kufanyika kwenye kilimo ambapo Profesa Mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya mkakati wa Serikali ya awamu ya sita kuwekeza zaidi kwenye kilimo, huku Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Profesa Haji Semboja amesema Tanzania inatambulika duniani kwa fursa nyingi kwenye kilimo. Read More