Uchaguzi Mkuu 2025
-
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndugu Samia Suluhu Hassan Mei 30 mwaka huu ameongoza chama hicho kuzindua Ilani ya Uchaguzi (2025-2030) ambayo imebeba ajenda tisa, ambazo ni matamanio ya wananchi ambayo wamekuwa wakitaka kuona serikali ikiyafanyia kazi ili kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo ya Taifa. Katika kipindi hicho cha miaka mitano, lengo kuu la serikali litakuwa kukuza uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi. Ili kufikia lengo hilo, mkazo mkubwa utawekwa katika maeneo tisa ambayo ni, kuchochea mapinduzi ya kiuchumi, kuzalisha ajira, kuboresha maisha ya wananchi, kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kukuza matumizi ya sayansi na teknolojia, kudumisha amani, utulivu na usalama, kudumisha utamaduni na kukuza sanaa na michezo na kuongeza kasi ya maendeleo vijijini. Ni wazi kuwa, maeneo yote tisa yanagusa maisha ya wananchi, na hili linadhihirisha dhamira ya Dkt. Samia katika kuendelea na mageuzi kwa lengo la kutokomeza umaskini, kuinua hali za maisha ya Watanzania wote na kuinua ustawi wa jamii na Taifa letu. Amewahakikisha wananchi kuwa, kutokana na mafanikio makubwa ambayo CCM imeyapata katika utekelezaji wa ilani ya mwaka 2020-2025, ni wazi kuwa inauwezo wa kutekeleza ilani mpya, ambayo imetengezwa kwa weledi mkubwa ikijumuisha maoni ya wananchi na wadau mbalimbali pamoja na mapendekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. “Kubwa kwa Watanzania, ni kuweka utulivu ndani ya nchi yetu, kufanya kazi kwa bidhii,” amesema Dkt. Samia huku akiwaasa wananchi kumwomba Mwenyezi Mungu awasaidie kufanikisha yote waliyojipangia. Wananchi na taasisi zilizotoa maoni yao kuhusu ilani hiyo wamekipongeza chama hicho kuwa kimezingatia maoni yaliyotolewa, ambayo kwa muda mrefu yalikuwa ni matamanio ya wananchi ikiwemo suala la Katiba Mpya ambapo chama hicho kimeahidi kuhuisha na kukamilisha mchakato wa katiba hiyo. Read More