UCHAGUZI CCM
-
Mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alisema bila CCM imara nchi itayumba kwa kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyaona au kuyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho. Nia hiyo ya Mwalimu Nyerere ya kuona chama kikiwa imara yanaendelezwa na mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amewasihi wanachama kurejea na kuwa wamoja baada ya kumalizika kwa chaguzi ndani ya chama ili kukiwezesha chama kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuisimamia Serikali kwenye utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/25. “Haitakuwa rahisi hata kidogo kwa CCM kutekeleza kwa ufanisi malengo yake […] iwapo wanachama na viongozi hatutakuwa wamoja na tulioshikamana kwa dhati,” amesema hayo huku akitoa rai kuwa “lengo la uchaguzi sio kutafuta ushindi wa mtu mmoja mmoja, bali ni makakati wa kujiimarisha na kujipanga kwa ajili ya kutafuta ushindi wa chama chetu katika chaguzi zijazo.” Aidha, amesema utekelezaji wa wa ilani ya chama hicho unakwenda vizuri na kwa kasi kubwa na kwamba wanaotaka kupima utekelezaji wake, wapime wakijua kwamba hadi sasa ni miaka miwili tu imepita tangu uchaguzi ufanyike. Amesisitiza kuwa CCM ni mfano wa kuigwa na vyama vingine, hivyo sheria kanuni na taratibu lazima zifuatwe, huku akimtaka kila mwanachama kuzingatia wajibu kama ilivyoainishwa kwenye katiba yake ili kuiendeleza CCM inayoamini katika haki, usawa na amani na maendeleo ya Taifa. Read More