Sekta ya Kilimo
-
Tanzania imeweka mkakati wa kutumia mageuzi ya kilimo kupunguza umaskini wa wananchi ikizingatiwa kuwa takribani asilimia 70 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo. Akizungumza katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Usalama wa Chakula, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu amesema Tanzania imekuja na Ajenda ya 10/30 ambayo inalenga kuwezesha kilimo kukua kwa asilimia 10, kutoka asilimia 4 ya sasa, ifikapo mwaka 2030. Mheshimiwa Rais ametaja hatua ambazo Serikali imechukua na inaendelea kuchukua ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio vya kikodi kwa sekta binafsi ili ishiriki kikamilifu kwenye kilimo. Vivutio hivyo ni pamoja na kutoa punguzo la kodi (capital allowance) kwa asilimia 100, kusamehe ushuru wa forodha na kodi ya ongezeko la thamani katika vifaa vya kilimo ikiwemo vya vifaa vitakavyotumika katika umwagiliaji, uongezaji thamani, kulima na nishati salama, hatua ambayo inalenga kupunguza gharama za uwekezaji. Hatua nyingine ni Mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kufanya kilimo cha kisasa, mradi ambao utawezesha kuongeza uzalishaji na kutunza mazingira. “Kutunza mazingira bila kupunguza umaskini tutakuwa tunafanya kazi bure,” amesema huku akiongeza kuwa kazi ya Serikali ni kuwapa vijana mafunzo na ardhi, hivyo sasa sekta binafsi inatakiwa iingie kwenye kutoa fedha, lakini pia mitambo kufanya kilimo chetu kiwe cha kisasa Pia, amebainisha kuwa mkazo umewekwa katika tafiti ili kuwezesha wananchi kufanya kilimo chenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko, ukame, wadudu na kutunza mazingira. Katika eneo hili Serikali imejenga na inahamasisha sekta binafsi kujenga skimu za umwagiliaji na mabwawa ya kuvuna maji ya mvua. “Sekta binafsi itakuwa na kazi ya kuhakikisha wanaongeza thamani mazao yote yanayozalishwa, lakini pia biashara ya kilimo,” amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza kuwa katika hili Serikali inahakikisha upatikanaji wa ardhi na utoaji wa leseni na vibali kwa wawekezaji wanaotaka kuingia kwenye kilimo cha… Read More
-
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema sekta ya kilimo nchini inatarajiwa kukua kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 ikilinganisha na ukuaji wa sasa wa takribani asilimia 3.6. Akizungumza kwenye mdahalo wa ‘Food Action Partnership: Investing in Greater Resilience’ nchini Uswisi amesema Tanzania imetengeneza fursa za kitaifa kwa ajili ya mabadiliko ya mfumo wa chakula unaotarajia kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha maisha ya watu na kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika kudhibiti mfumo endelevu wa chakula nchini, Rais Samia amesema jitihada kadhaa zimefanyika, ikiwemo kuanzisha mradi kwa ajili ya vijana huku wakiendelea kuimarisha ukuaji wa shoroba za kilimo pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo mara 4 ukilinganisha na ile iliyopita. Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza miradi na mafunzo mbalimbali ya kilimo kwa vijana ili kuongeza tija kwenye kilimo na kuwezesha vijana kushiriki kwenye uchumi wa Tanzania ambapo lengo ni kuzalisha ajira milioni 1 ifikapo mwaka 2025. Mdahalo huo uliohudhuriwa na zaidi ya viongozi 50 kutoka Afrika, Asia, Ulaya na Marekani mbali na Rais Samia wachangiaji wengine walikuwa Rais Gustavo Petro wa Colombia, Tran Hong Ha, Naibu Waziri Mkuu wa Vietnam na Alvaro Lario, Rais wa Wakfu wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Roma. Read More