Samia Suluhu

  • Watalii wafurika nchini miezi iliyotambuliwa kama ‘low season’ miaka ya nyuma

    Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu hali ya uchumi kwa Mei 2024 imeonesha kuwa watalii wameendelea kumiminika nchini ambapo miezi ya Machi na Aprili ambayo ilitambulika huko nyuma kwa kuwa na idadi ndogo ya watalii (low season), kwa mwaka 2024 watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 21.9 na asilimia 21.8 mtawalia ikilinganishwa na miezi kama hiyo mwaka jana. Hali hii ambayo ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini na duniani inaifanya sekta hiyo kuendelea kuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni ambapo katika miezi hiyo utalii umeingiza dola za Marekani bilioni 3.58 kwa Machi na dola za Marekani bilioni 5.75 kwa Aprili kutoka dola za Marekani bilioni 2.7 na dola za Marekani bilioni 2.8, mtawaliwa kwa miezi kama hiyo mwaka jana 2023. Mafanikio haya yametokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali pamoja na sekta binafsi ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii nje ya nchi, huduma bora kwa wageni wanaofika kutalii nchini pamoja na kuimarisha huduma za usafiri, mathalani sekta ya anga. Ripoti ya BoT inaunga mkono utafiti uliofanywa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kwa robo ya Januari-Machi 2024, ambapo kwa ukuaji unaoendelea sasa wa sekta ya utalii, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani kwa ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya UVIKO-19, yaani mwaka 2019. Mafanikio na kuimarika kwa sekta ya utalii, pamoja na sekta nyinginezo kama madini, usafirishaji, kilimo kutaendelea kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 5.8 mwaka huu.   Read More

  • Tanzania yazidi kujiimarisha kuwa kitovu cha biashara eneo la Maziwa Makuu

    Tanzania inaendelea kujiimarisha katika mkakati wa kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji pamoja na biashara ambapo leo imesaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha sita cha reli ya kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma (506km) kwa gharama ya TZS trilioni 5. Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema kuwa “hilo litafanikiwa tukihakikisha miradi yote tunayoitekeleza, tunaisimamia na kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.” Ujenzi wa kipande cha Tabora – Kigoma ambacho kitaungana na kipande cha Uvinza-Musongati-Kindu itaiunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DCR), upande wa mashariki ambapo kuna mizigo mingi inayohitaji kusafirishwa kwenda na kutoka Bandari ya Dar es Salaam, ikifahamika kuwa mwaka 2021 taifa hilo lilipitisha mizigo ya tani milioni 2.4 katika bandari hiyo. Aidha, ujenzi wa reli hiyo utachochea ukuaji wa biashara kwa kupunguza gharama za kusafirisha mizigo kwenda DRC ambapo sasa gharama za kusafirisha kontena moja hufika hadi TZS milioni 35, huku ikichukua hadi mwezi mmoja. Kuanza kutumika kwa reli kutapunguza muda na gharama hadi kufikia TZS milioni 9 na muda wa siku moja, huku ukiwa usafiri ulio salama zaidi. “Takwimu zinaonesha ujenzi wa reli hii utasaidia kufungua maeneo yenye machimbo ya madini yenye mzigo wa zaidi ya tani milioni 150 na mizigo mingine ya kuwezesha migodi hiyo kufanya kazi,” ameeleza Dkt. Samia. Mbali na hayo ujenzi wa reli umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya wananchi 20,000 wamepata ajira za moja kwa moja, huku waajiriwa wakilipwa TZS bilioni 237.7. Pia umetoa zabuni kwa Watanzania zenye thamani ya takribani trilioni 2 na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya kodi TZS bilioni 949. Read More