Samia Suluhu
-
Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kujikwamua kiuchumi ambapo serikali yake ikitangaza mikakati nane inayolenga kukuza uwekezaji kwa mwaka 2025/26, vijana wamepewa kipaumbele ili kuwa miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini. Moja ya hatua ambayo Serikali imepanga kuchukua ni kuanzisha kituo cha kuhudumia na kuwezesha wawekezaji vijana ambacho kitatoa huduma za mafunzo, uwezeshaji na usaidizi. Kituo hicho kinatarajiwa kuanzishwa kabla mwaka huu haujaisha ambapo makao makuu yake yatakuwa Dar es Salaam, huku kikiwa na uwakilishi wa maeneo yote. Aidha, sambamba na hilo serikali inakusudia kuanzisha programu maalum ya kuwezesha wawekezaji vijana kubuni na kuanzisha uwekezaji wa viwandani. Programu hiyo itahusisha mafunzo, uwezeshaji wa kupewa ardhi, kuunganishwa na wauzaji wa mitambo na malighafi na benki. Kwa kuanza maeneo yaliyotengwa kwa vijana yapo Nala, Dodoma; Bunda, Mara; Songea, Ruvuma; na Bagamoyo. Pwani. Hatua hizi zinachukuliwa ikiwa ni mwendelezo wa kufungua fursa kwa vijana kujiajiri na kuajiriwa. Mkakati mwingine uliochukuliwa ni Mheshimiwa Rais Samia kuunda wizara maalum ya vijana ili masuala yao yashughulikiwe kwa uharaka. Mheshimiwa Rais amekuwa akisisitiza kuwa ana imani na vijana na kwamba wao ni sehemu muhimu ya maendeleo ya nchi. Read More
-
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu hali ya uchumi kwa Mei 2024 imeonesha kuwa watalii wameendelea kumiminika nchini ambapo miezi ya Machi na Aprili ambayo ilitambulika huko nyuma kwa kuwa na idadi ndogo ya watalii (low season), kwa mwaka 2024 watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 21.9 na asilimia 21.8 mtawalia ikilinganishwa na miezi kama hiyo mwaka jana. Hali hii ambayo ni matokeo ya kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini na duniani inaifanya sekta hiyo kuendelea kuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni ambapo katika miezi hiyo utalii umeingiza dola za Marekani bilioni 3.58 kwa Machi na dola za Marekani bilioni 5.75 kwa Aprili kutoka dola za Marekani bilioni 2.7 na dola za Marekani bilioni 2.8, mtawaliwa kwa miezi kama hiyo mwaka jana 2023. Mafanikio haya yametokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali pamoja na sekta binafsi ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii nje ya nchi, huduma bora kwa wageni wanaofika kutalii nchini pamoja na kuimarisha huduma za usafiri, mathalani sekta ya anga. Ripoti ya BoT inaunga mkono utafiti uliofanywa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kwa robo ya Januari-Machi 2024, ambapo kwa ukuaji unaoendelea sasa wa sekta ya utalii, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani kwa ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya UVIKO-19, yaani mwaka 2019. Mafanikio na kuimarika kwa sekta ya utalii, pamoja na sekta nyinginezo kama madini, usafirishaji, kilimo kutaendelea kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 5.8 mwaka huu. Read More
-
Tanzania inaendelea kujiimarisha katika mkakati wa kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji pamoja na biashara ambapo leo imesaini mkataba na mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha sita cha reli ya kisasa kutoka Tabora hadi Kigoma (506km) kwa gharama ya TZS trilioni 5. Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia amesema kuwa “hilo litafanikiwa tukihakikisha miradi yote tunayoitekeleza, tunaisimamia na kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.” Ujenzi wa kipande cha Tabora – Kigoma ambacho kitaungana na kipande cha Uvinza-Musongati-Kindu itaiunganisha Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DCR), upande wa mashariki ambapo kuna mizigo mingi inayohitaji kusafirishwa kwenda na kutoka Bandari ya Dar es Salaam, ikifahamika kuwa mwaka 2021 taifa hilo lilipitisha mizigo ya tani milioni 2.4 katika bandari hiyo. Aidha, ujenzi wa reli hiyo utachochea ukuaji wa biashara kwa kupunguza gharama za kusafirisha mizigo kwenda DRC ambapo sasa gharama za kusafirisha kontena moja hufika hadi TZS milioni 35, huku ikichukua hadi mwezi mmoja. Kuanza kutumika kwa reli kutapunguza muda na gharama hadi kufikia TZS milioni 9 na muda wa siku moja, huku ukiwa usafiri ulio salama zaidi. “Takwimu zinaonesha ujenzi wa reli hii utasaidia kufungua maeneo yenye machimbo ya madini yenye mzigo wa zaidi ya tani milioni 150 na mizigo mingine ya kuwezesha migodi hiyo kufanya kazi,” ameeleza Dkt. Samia. Mbali na hayo ujenzi wa reli umeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya wananchi 20,000 wamepata ajira za moja kwa moja, huku waajiriwa wakilipwa TZS bilioni 237.7. Pia umetoa zabuni kwa Watanzania zenye thamani ya takribani trilioni 2 na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya kodi TZS bilioni 949. Read More